Raisi: Makubaliano yatafikiwa iwapo Iran itaondolewa vikwazo
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema iwapo Marekani italiondolea vikwazo haramu taifa la Iran, basi mazingira yatakuwa yameandaliwa kwa ajili ya kufikia makubaliano katika mazungumzo yanayonuia kufufua makubaliano ya JCPOA huko Vienna.
Sayyid Ebrahim Raisi alisema hayo jana Jumatatu katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Pekka Haavisto, Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland na kuongeza kuwa, "tumeshasema mazingira yatakuwa tayari kwa ajili ya kufikiwa makubaliano, iwapo vikwazo vitafutwa, Tehran imedhihirisha kuwa inatekeleza wajibu wake, ila hatutafungamanisha uchumi wetu na JCPOA."
Amesema anatumai nchi za Ulaya zitafuata njia ya uhuru wa kujikomboa kwenye ubeberu wa Marekani kwa kuwa Washington katu haiwezi kuaminika.
Kadhalika Rais wa Iran amesema uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Finland umeimarika pakubwa tangu baada ya Mapinduzi ya Kiislamu, lakini ushirikiano huo haupaswi kuathiriwa na maajinabi.
Kabla ya hapo, Pekka Haavisto, Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland alikutana na kufanya mazungumzo ya mwenzake wa hapa Iran, Hossein Amir-Abdollahian, ambapo walijadili suala la kuboreshwa uhusiano wa pande mbili hususan katika nyuga za sayansi, teknolojia, Vyuo Vikuu, na maji ya kunywa kupitia nishati ya miale ya jua.
Haavisto ameashiria miaka 90 ya uhusiano wa Iran na Finland na kueleza kuwa, nchi yake inachukulia kwa uzito maalumu uhusiano wa pande mbili na kusisitiza kuwa kuna fursa nyingi za kuuboresha zaidi.
Aidha amesema ni jambo la kusikitisha kwamba Wamarekani walijiondoa kwenye JCPOA, na kueleza kuwa haridhishwa na hatua za Washington mkabala wa mapatano hayo ya kimataifa.