Chanjo ya Iran ya Razi Cov Pars yabainika kuwa na uwezo mkubwa
Chanjo ya COVID-19 ya Razi Cov Pars iliyotengenezwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imebainika kuwa na uwezo mkubwa na nchi kadhaa tayari zimeshaiagiza.
Chanjo ya Razi Cov Pars imetengenezwa na Taasisi ya Utafiti wa Chanjo ya Razi na baada ya kupita miaka miwili ya utafiti na majaribio, sasa imeanza kutumiwa katika zoezi la chanjo ya COVID-19 nchini Iran. Kutokana na kubainika kuwa chanjo hiyo ina uwezo mkubwa kuliko baadhi ya chanjo zilizoingizwa nchini, hivi sasa nchi kadhaa za kigeni zimeshatuma maombi ya kununua chanjo hiyo.
Daktari Ali Ishaq, mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Chanjo ya Razi amezungumza kuhusu chanjo hiyo ya Razi Cov Pars na kusema: "Kwa mtazamo wa kinga ya seli, chanjo hii inaibua kinga ya asilimi 75."
Taasisi ya Utafiti wa Chanjo ya Razi ina historia ndefu ya uzalishaji chanjo na baada ya janga la COVID-19 kuripotiwa duniani ilianza mkakati wa kuzalisha chanjo ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Mwezi Septemba, Mohammad Hossein Fallah Mehrabadi, mkuu wa utafiti na teknolojia katika Taasisi ya Utafiti wa Chanjo ya Razi alitangaza kuanza awamu ya tatu ya majaribio kwa wanadamu ya chanjo ya Razi Cov Pars katika mikoa ya Tehran na Alborz na kuwajumuisha watu 40,000 waliojitolea.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa makadirio wataweza kuzalisha chanjo milioni 15 hadi millioni 20 za chanjo ya Razi Cov Pars hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu.
Chanjo hii ni ya aina yake kwani ina dozi tatu ambazo ni kwa mujibu wa maagizo ya Shirika la Afya Duniani (WHO). Dozi za kwanza mbili ni za kudungwa na dozi ya tatu ni tone linaloingizwa mwilini kupitia pua.
Iran iko mbioni kujitegenezea chanjo za COVID-19 na tayari chanjo kadhaa zilizotengenezwa nchini zimeanza kutumika. Chanjo hizo ni pamoja na COVIran Barekat iliyotegenezwa na Taasisi ya Utekelezaji Maagizo ya Imam Khomeini (MA) na ile ya PastoCoVac, ambayo imeundwa kwa ushirikiano wa taasisi ya Pasteur ya Iran na Taasisi ya Finlay na Cuba. Chanjo nyingine ambayo hivi karibuni imeanza kutumika nchini Iran ni ile ya Spikogen ambayo imetengenezwa kwa ushirikiano baina ya shirika la CinnaGen la Iran na shirika la Vaxine la Australia.
Chanjo hizo zinasubiri idhini ya Shirika la Afya Duniani kuanza kuuzwa katika soko la kimataifa. Chanjo zingine za Iran ambazo zingali zinafanyiwa majaribio ya mwisho ni Noora na Fakhra.