Bagheri Kani: Tunakaribuia zaidi kufikia mapatano ya nyuklia Vienna
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i80448-bagheri_kani_tunakaribuia_zaidi_kufikia_mapatano_ya_nyuklia_vienna
Kiongozi wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia ya Vienna amesema kuwa, pande mbili zinakaribia kufikia mapatano baada ya wiki kadhaa ya mazungumzo ya kina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 17, 2022 04:33 UTC
  • Ali Bagheri Kani
    Ali Bagheri Kani

Kiongozi wa timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia ya Vienna amesema kuwa, pande mbili zinakaribia kufikia mapatano baada ya wiki kadhaa ya mazungumzo ya kina.

Ali Bagheri Kani aliandika jana kwenye mtandao wa Twitter kuhusu mwenendo wa mazungumzo ya Vienna kwamba: "Baada ya wiki kadhaa za mazungumzo ya kina, tumekaribia makubaliano kuliko hapo awali, lakini hakuna kilichokubaliwa hadi kila kitu kitakapokubaliwa."

Bagheri Kani ameongeza kuwa, kutilia maanani uhakika wa mambo, kujiepusha na tabia ya kupenda makuu na uzoefu wa miaka 4 iliyopita ni muhimu ili kufikia lengo hili."

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir Abdollahian Jumanne iliyopita aliashiria mazungumzo yake na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Joseph Borell na kusema kuwa, mienendo ya kiuwajibikaji ya upande wa Magharibi ndio sharti la kufikiwa makubaliano ya mwisho katika mazungumzo ya Vienna.

Mazungumzo ya Vienna

Kwa kuzingatia ukiukaji makubaliano ya JCPOA uliofanywa na Marekani tangu siku za awali za utekelezaji wa mapatano wakati wa urais wa Barack Obama, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza katika duru zilizopita za mazungumzo ya sasa ya Vienna kuhusu ulazima wa kuwepo "hakikisho la kudumu makubaliano" na "uthibitisho wa kuondolewa vikwazo", yakiwa ndio matakwa yake mawili makuu ya kutekeleza tena kikamilifu makubaliano ya JCPOA.

Duru ya nane ya mazungumzo ya uondoaji vikwazo ilianza mjini Vienna tarehe 27 Desemba; na baada ya kusitishwa kwa kipindi kifupi ili pande husika ziende kufanya mashauriano katika miji yao mikuu, ilianza tena tarehe 8 ya mwezi huu wa Februari, katika mji mkuu huo wa Austria.