Iran yajibu ripoti iliyopotoshwa kuhusu mazungumzo ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i80480-iran_yajibu_ripoti_iliyopotoshwa_kuhusu_mazungumzo_ya_jcpoa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, usiku wa kuamkia leo Ijumaa amejibu ripoti iliyopotoshwa kuhusu mazungumzo ya Vienna ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kusisitiza kuwa, makubaliano ya mwisho yatakuwa tofauti kabisa na uvumi unaoenezwa kuhusu kurejea Marekani kwenye mapatano hayo.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Feb 17, 2022 23:42 UTC
  • Iran yajibu ripoti iliyopotoshwa kuhusu mazungumzo ya JCPOA

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, usiku wa kuamkia leo Ijumaa amejibu ripoti iliyopotoshwa kuhusu mazungumzo ya Vienna ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kusisitiza kuwa, makubaliano ya mwisho yatakuwa tofauti kabisa na uvumi unaoenezwa kuhusu kurejea Marekani kwenye mapatano hayo.

Majibu hayo yametolewa na Iran muda mchache baada ya shirika la habari la Reuters la Uingereza kudai kuwa limepata nakala ya kurasa 20 ya kile lilichodai ni makubaliano ya Vienna.

Shirika la habari la Iran Press limemnukuu Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran akisema kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, kitendo cha kuvipa vyombo vya habari taarifa zisizo sahihi ni jambo la hatari sana. Amesema, tusubiri kuona uvumi mwingine mwingi ukienezwa wakati huu wa kukaribia kufikiwa makubaliano rasmi katika mazungumzo hayo ya Vienna.

Mazungumzo ya JCPOA mjini Vienna, Austria

 

Awamu ya nane ya mazungumzo ya Vienna ambayo maudhui yake ni kuondolewa vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa Iran, iliendelea tena Jumanne ya Februari 8, 2022, baada ya kusimama kwa muda mfupi ili kutoa fursa kwa timu za mazungumzo kurejea katika nchi zao kwa mashauriano zaidi.

Awamu hiyo imeshuhudia maendeleo mazuri kutokana na mapendekezo mazuri ya Iran. Hata hivyo nchi za Magharibi ikiwemo serikali ya Joe Biden huko Marekani inaendelea kutekeleza vikwazo vya utawala uliopita wa nchi hiyo na hadi sasa nchi hizo za Ulaya na Marekani ndizo zinazozorotesha kufikiwa makubaliano ya mwisho huko Vienna.