Rais Ebrahim Raisi: Iran ina azma ya kupanua uhusiano wake na Serbia
Marais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Serbia wamesisitiza hamu na shauku kubwa ilizonazo nchi zao ya kupanua uhusiano baina yao katika nyanja mbalimbali
Marais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Aleksandar Vučić wa Serbia wamesema hayo katika mazungumzo yao kwa njia ya simu ambapo wameashiria uwezo mkubwa zilionazo nchi zao ambao unaweza kutumiwa kwa ajili ya kustawisha zaidi ushirikiano huo.
Viongozi hao wamesisitiza kwamba, Tehran na Belgarde zina uwezo tofauti ambao unaweza kufanywa kuwa chachu ya kustawisha zaidi ushirikiano katika sekta mbalimbali hususan katika uchumi na masuala ya biashara.
Sayyid Ebrahim Raisi Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo yake na Rais Aleksandar Vučić wa Serbia kwamba, Tehran ina azma thabiti ya kukuza ushirikiano wake na Belgrade katika mkondo wa maslahi ya pande mbili.
Ebrahim Raisi ameashiria pia fursa na uwezo tofauti wa nchi mbili hizi kwa ajili ya kuinua kiwango cha ushirikiano na kusema kwamba, kupanuliwa ushirikiano wa pamoja hususan katika uga wa kiuchumi, kibiashara na kiuchumi ni hatua yenye manufaa ya pande mbili ambapo kuna haja ya kutambuliwa fursa na kisha kufanyiwa kazi.
Kwa upande wake Rais Aleksandar Vučić wa Serbia amesema kuwa, nchi yake inafuatilia kwa moyo wote suala la kuinua kiwango cha uhusiano na ushirikiano wa kibiashara na kimasoko na Tehran sambamba na kuimarisha mahusiano ya kisiasa na ya kimkakati.