Iran kuendelea kurutubisha urani kwa 20% hata ikiondolewa vikwazo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i80768-iran_kuendelea_kurutubisha_urani_kwa_20_hata_ikiondolewa_vikwazo
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuzalisha madini ya urani iliyoritubishwa kwa kiwango cha asilimia 20, hata kama itaondolewa vikwazo katika mazungumzo ya Vienna yanayolenga kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Feb 25, 2022 23:09 UTC
  • Iran kuendelea kurutubisha urani kwa 20% hata ikiondolewa vikwazo

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuzalisha madini ya urani iliyoritubishwa kwa kiwango cha asilimia 20, hata kama itaondolewa vikwazo katika mazungumzo ya Vienna yanayolenga kuhuisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Mohammad Eslami alinukuliwa akisema hayo jana Ijumaa na shirika la habari la Fars na kueleza kuwa, "kurutubisha urani kwa kiwango kisichozidi asilimia 60 kunaendelea, na hatua hii iliwalazimisha Wamagharibi waende mbio kwenye meza ya mazungumzo."

Eslami ameeleza bayana kuwa, "hata baada ya kuondolewa vikwazo vyote, na kufufuliwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA ya mwaka 2015, Iran itaendelea kurutubisha urani kwa kiwango cha asilimia 20.

Katika mapatano hayo, Iran ilikuwa imeafikia kurutubisha madini hayo kwa asilimia 3.67 pekee, lakini ililazimika kutazama upya msimamo huo baada ya Marekani kujiondoa kwenye makubaliano hayo ya kimataifa mwaka 2018, huku nchi za Ulaya zikifeli kuchukua hatua yoyote ya maana ya kuinusuru JCPOA.

Kiwanda cha kurutubisha urani cha Iran

Eslami amekumbusha kuwa, mwaka jana Iran ilikabidhi barua ya kuanza mipango ya uzalishaji wa urani iliyorutushwa kwa asilimia 60 kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA). Ifahamike kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa nchi chache duniani zenye uwezo wa kurutubisha urani kwa kiwango hicho cha hadi asilimia 60.

Shirika la Atomiki la Iran limekuwa likisisitiza kuwa linaweza kurutubisha madini ya urani hadi kiwango cha asilimia 90 bila tatizo lolote, na kwamba shughuli zote za nyuklia za Iran zinafanyika kwa malengo ya amani.