Amir-Abdollahian: Ikiwa Marekani itazingatia uhalisia wa mambo tutafikia mwafaka mzuri
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema "ikiwa Marekani itazingatia uhalisia wa mambo tutaweza kufikia mwafaka mzuri, imara na wa kudumu kwa uungaji mkono wa pande zote katika mazungumzo ya Vienna."
Hossein Amir-Abdollahian, ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi.
Katika mazungumzo hayo, Amir-Abdollahian na Wang Yi wamejadili hatua ya karibuni iliyofikiwa katika mazungumzo ya Vienna, ambapo waziri wa mambo ya nje wa Iran amesisitiza kuwa muelekeo wa China ni chanya na athirifu.
Akiashiria pia umuhimu wa uhusiano wa Iran na China, waziri Amir-Abdollahian ametilia mkazo pia kustawishwa uhusiano wa pande mbili katika nyanja zote akisema, hilo ni miongoni mwa mihimili mikuu na vipaumbele katika sera za nje za serikali ya Iran.
Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia mazungumzo aliyofanya mjini Moscow na waziri wa mambo ya nje wa Russia Sergey Lavrov na akaeleza kwamba, wamebadilisha mawazo juu ya maudhui mbalimbali na kwamba Moscow inatoa mchango chanya na kuunga mkono kuondolewa vikwazo ilivyowekewa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Halikadhalika, kutokana na uamuzi wa kuitishwa mkutano wa tatu wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi jirani na Afghanistan huko China; na katika kuitikia mwaliko aliopewa na mwenzake wa Beijing, Amir-Abdollahian ametangaza utayari wa kuhudhuria mkutano huo.
Katika mazungumzo hayo ya simu ya mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na China, Wang Yi amesema nchi yake inaunga mkono kwa kila hali mchakato wa mazungumzo ya Vienna na akasisitiza kuwa Beijing inaunga mkono kukamilishwa mazungumzo hayo kwa ajili ya kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran../