Miradi ya nyuklia ya Iran katika njia ya ustawi na maendeleo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i8179-miradi_ya_nyuklia_ya_iran_katika_njia_ya_ustawi_na_maendeleo
Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Iran ametangaza habari ya kuandaliwa mazingira mazuri ya kuzalishwa isotopu (atomu zenye uzito tofauti na atomu nyingine) endelevu kwa ushirikiano na Russia katika taasisi za nyuklia za Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 31, 2016 07:21 UTC
  • Dk Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Taasisi ya Atomiki ya Iran
    Dk Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Taasisi ya Atomiki ya Iran

Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Iran ametangaza habari ya kuandaliwa mazingira mazuri ya kuzalishwa isotopu (atomu zenye uzito tofauti na atomu nyingine) endelevu kwa ushirikiano na Russia katika taasisi za nyuklia za Iran.

Ali Akbar Salehi alisema hayo jana Jumatatu pembeni mwa kutiwa saini mkataba wa ushirikiano baina ya taasisi hiyo na kitengo cha utafiti wa nishati ya mafuta humu nchini kwa ajili ya kustawisha miradi yake ya atomiki katika taasisi za nyuklia za Fardo za Iran. Amesema: Kama tulivyoahidi, tumefanikiwa kuandaa uwanja wa kuzalisha isotopu endelevu na hivi sasa tunashirikiana na Warusi kwa ajili ya kuimarisha mashinepewa maalumu za kuzalisha aina hizo za isotopu. Ameongeza kuwa, ni kwa sababu hiyo ndio maana hivi sasa tunaimarisha mashinepewa aina ya Ir1 ambazo ndizo zenya uwezo wa kuzalisha isotopu za aina hiyo. Salehi ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, Iran haikuishia kwenye utengenezaji wa mashinepewa, bali kila leo taifa hili linazidi kujiimarisha katika upande wa taarifa na utaalamu wa masuala ya nyuklia. Kudhaminiwa mashinepewa zinazohitajiwa na sekta ya mafuta kwa ajili ya kutenganisha mafuta na mawe pamoja na kufanya utafiti katika uwanja huo na vile vile kutumia mada nururishi kwa ajili ya kugundua visima vya mafuta na kuvifanyia tathmini, ni miongoni mwa masuala ambayo yameandaa uwanja wa kuanza ushirikiano baina ya Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran na vitengo vya elimu, ufundi na utafititi nchini. Aidha Iran imefanikiwa kujizalishia mashinepewa inazohitajia kwa ajili ya sekta ya afya na matibabu ambazo zina umuhimu mkubwa katika kuzalisha chanjo na dawa zenye michangayiko mipya tofauti. Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran amezungumzia pia suala la kuuzwa mafuta mazito ya nyuklia ya Iran yaliyozidi katika matumizi ya Tehran na kusema kuwa, mazungumzo yanaendelea vizuri hivi sasa baina ya Iran na washitiri tofauti na kwamba Warusi wamesema wako tayari kununua tani 40 za maji hayo mazito ya nyuklia ya Iran, ingawa mazungumzo bado hayajakamilika. Kwa mujibu wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Iran imeahidi kuuza tani 130 za maji yake mazito yaliyozidi katika matumizi yake. Si hayo tu, lakini pia Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran imefanikiwa kuzalisha asilimia 20 ya fueli nyuklia inayohitajiwa na vinu vyake na hivi sasa kinu cha utafiti wa nyuklia cha Tehran kinaendeshwa na fueli iliyozalishwa ndani ya Iran. Marekani na nchi kadhaa za Ulaya kwa miaka mingi zilikuwa zikipiga makelele yasiyo na mashiko kwamba miradi ya nyuklia ya amani ya Iran eti ni hatari kwa usalama wa dunia. Madola hayo ya kiistikbari yalikuwa yanadai kuwa Iran ina nia ya kumiliki silaha angamizi za atomiki. Lengo la njama hizo zilikuwa ni kuikwamisha kikamilifu Iran katika juhudi zake za kumiliki teknolojia hiyo muhimu sana. Hata hivyo hatimaye madola hayo yamelazimika kukiri kuwa Iran ina haki ya kumiliki teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani, baada ya kupata yakini kuwa, hayawezi kulizua taifa hili kumiliki teknolojia hiyo tena kwa kutegemea wataalamu wake lenyewe. Fauka ya hayo, baadhi ya nchi zinazounda kundi la 5+1 zimeamua kushirikiana na Iran katika utafiti wa maendeleo ya nyuklia na ndio maana hivi sasa nusu ya taasisi za nyuklia za Fardo za Iran zimekuwa maalumu kwa ajili ya uzalishaji wa isotopu endelevu ambazo ni muhimu katika sekta za viwanda, kilimo na tiba. Ukweli wa mambo ni kuwa, nguvu za kitekonolojia za Iran kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu ndizo zilizolifanya taifa hili kupata haki zake za nyuklia na si fadhila kutoka kwa madola ya kibeberu.