SEPAH: Adui ana kiwewe kikubwa kwa kuona mshikamano katika majeshi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i82704-sepah_adui_ana_kiwewe_kikubwa_kwa_kuona_mshikamano_katika_majeshi_ya_iran
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema wakati alipoonana na Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu kwamba umoja na mshikamano wa vikosi vya ulinzi vya Iran unamtia kiwewe adui.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Apr 19, 2022 22:43 UTC
  • SEPAH: Adui ana kiwewe kikubwa kwa kuona mshikamano katika majeshi ya Iran

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesema wakati alipoonana na Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu kwamba umoja na mshikamano wa vikosi vya ulinzi vya Iran unamtia kiwewe adui.

Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH jana Jumanne alionana na Meja Jenerali Abdul Rahim Mousavi, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu humu nchini na kusisitiza kuwa, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limepiga hatua kubwa katika nyuga zote kwa nguvu na uimara wa hali ya juuu. Mazungumzo hayo yamefanyika kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Naye Meja Jenerali Mousavi, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu amesema, umoja na mshikamano imara baina ya majeshi ya Iran unazipa furaha kubwa nyoyo za wapenda haki na kuongeza kuwa, suala la kujitosheleza Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu lina historia ndefu na mchakato wa kujiimarisha na kujitegemea zaidi unaendelea kwa kasi kubwa.

Meja Jenerali Hossein Salami (kushoto) akiwa pamoja na Meja Jenerali Mousavi, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu

 

Kiujumla vikosi vya ulinzi wa Iran vinajitegemea na viko imara kiasi kwamba adui hivi sasa hana uthubutu wa kuanzisha vita vya moja kwa moja na Jamhuri ya Kiislamu. Hii ni kusema kuwa, juzi Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH lilitangaza kuwa, ndege mpya isiyo na rubani iliyopewa jina la Ghaza, imefaulu katika majaribio ya kuendesha operesheni zake na sasa inafanya kazi kikamilifu.

Ndege hiyo kubwa ya kivita isiyo na rubani, ambayo ilizinduliwa mwezi Mei mwaka jana, ina mbawa zenye urefu wa mita 21 na uwezo wa kubeba mzigo wa kilo 500. Droni ya Ghaza inaweza kuruka angani kwa masaa 35 bila ya kusita.