Jeshi la Iran lazindua trela ya kubeba vifaru iliyoundwa nchini
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limezindua trela ndefu yenye uwezo wa kubebe vifaru ambayo imeundwa kikamilifu na wataalamu wa Iran.
Trela hiyo ijulikanayo kama Kian 600+ na ina uwezo wa kubeba vifaru na magari ya deraya. Uzinduzi huo ulifanyika Jumatano katika sherehe iliyohudhuriwa na Kamanda wa Jeshi la Iran Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi, Naibu Kamanda wa Jeshi la Iran Mohammad Hossein Dadras, Mratibu wa Jeshi la Iran Admeri Habibollah Sayyari na maafisa wengine wa ngazi za juu jeshini.
Siku ya Jumatatu pia Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilizindua zana mpya za kijeshi wakati wa Gwaride la Siku ya Kitaifa ya Jeshi. Katika gwaride hilo kulionyeshwa pia ndege mpya zisizo na rubani au drone ikiwemo ile ijulikanayo kama Ababil-5. Jeshi la Iran pia lilizindua makombora mapya yakiwemo ya Fath 360, Labeik, Dezul na Majid.
Katika miaka ya hivi kairbuni wataalamu wa kijeshi wa Iran wameweza kupata mafanikio makubwa katika uundaji wa zana za kijeshi na kivita na hivyo nchi hii imeweza kujitosheleza kaktika sekta ya ulinzi.
Iran imesisitiza mara kadhaa kuwa haitasita kuimarisha uwezo wake wa kijeshi ikiwa ni pamoja na uwezo wake wa makombora na kuongeza kuwa uwezo wa kijeshi ni kwa ajili ya kujihami.