Iran yawakamata majasusi watatu wa Mossad
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i82750-iran_yawakamata_majasusi_watatu_wa_mossad
Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran imetangaza kuwakamata majasusi watatu waliokuwa wakitumikia shirika la ujasusi la Israel, Mossad, katika mkoa wa Sistan na Baluchestan, Kusini Magharibi mwa nchi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 21, 2022 03:35 UTC
  • Iran yawakamata majasusi watatu wa Mossad

Wizara ya Usalama wa Taifa ya Iran imetangaza kuwakamata majasusi watatu waliokuwa wakitumikia shirika la ujasusi la Israel, Mossad, katika mkoa wa Sistan na Baluchestan, Kusini Magharibi mwa nchi.

Katika taarifa Jumatano usiku, wizara hiyo imesema majasusi hao wa Mossad wanahusika katika kusambaza taarifa na nyaraka za siri.

Majasusi hao wamekamatwa kufuatia amri ya mahakama lakini bado uraia wao haujatajwa.

Mwezi Julai mwaka jana Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Ujasusi cha wizara hiyo alisema vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu viliwatia nguvuni magaidi hao waliojipenyeza nchini kupitia mpaka wa magharibi.

Alieleza bayana kuwa, mbali na kukamatwa maajenti hao wa Mossad, lakini maafisa usalama nchini walifanikiwa pia kunasa idadi kubwa ya silaha na mada za miripuko zilizoingizwa nchini kimagendo na magaidi hao wenye mfungamano na Wazayuni.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Wizara ya Intelijensia ya Iran alisema majasusi hao wa Mossad ya Israel walitiwa mbaroni kutokana na kuwa macho vyombo vya usalama vya taifa hili.

Alisema baadhi ya silaha zilizonaswa katika oparesheni hiyo ni pamoja na bunduki za aina kadhaa ikiwemo ya AK-47, maguruneti, mada za miripuko na risasi.

Maafisa wa usalama Iran mwezi Machi pia walisambaratisha makundi mawili ya magaidi wanaopata himaya ya kigeni ambao walikuwa wanalenga kuwaua raia wa kigeni wanaofanya kazi katika miradi wa maendeleo katika mkoa wa Sistan na Baluchestan.