Ayatullah Hamedani: Wanaodai kutetea haki za binaadamu duniani wamefedheheka tena
-
Ayatullah Nouri Hamedani
Ayatullah Nouri Hamedani ambaye ni miongoni mwa viongozi wakuu wa kidini katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran amelaani kitendo cha kuvunjiwa heshima kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu, Qur'ani huko Sweden na Msikiti wa al Aqsa huko Quds Tukufu na vilevile mauaji ya watu wa Afghanistan.
Ayatullah Hamedani amesema katika ujumbe wake kwamba: Wanaotoa madai bandia ya kutetea haki za binaadamu kwa mara nyingine tena wameharibu heshima na hadhi zao kwa kuhalalisha kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na kunyamazia kimya jinai za Wazayuni maghasibu na hujuma ya kigaidi huko Afghanistan.
Kiongozi wa chama chenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia cha Stram Kurs (Hard Line) na waungaji mkono wake, walichoma moto nakala ya Qur'ani katika mji wa pwani ya Mashariki mwa Sweden wa Linkoping, suala ambalo lilisababisha ghasia na machafuko makubwa baina ya Waislamu na polisi.
Uhalifu huo uliofanywa kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza na kwa himaya wa polisi wa Sweden, umeibua hasira kubwa baina ya Waislamu kote duniani.
Ijumaa iliyopita (15 Aprili) pia wanajeshi wa utawala haramu wa Israel waliwashambulia Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ndani ya Msikiti wa al Aqsa huko Quds inayokaliwa kwa mabavu na kujeruhi Wapalestina wasiopungua 160. Waislamu wengine zaidi ya 400 wametiwa nguvuni.
Katika ujumbe wake, Ayatullah Hossein Nouri Hamedani amesema: Wanaotoa madaii ya uongo ya kutetea haki za binaadamu kwa mara nyingine tena wamechafua hadhi na heshima yao kwa kuhalalisha kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na kunyamazia kimya jinai za Wazayuni na hujuma ya kigaidi nchini Afghanistan.
Ameongeza kuwa: Leo hii Waislamu na wapigania uhuru wote duniani wanatakiwa kulaani matusi na kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na pia waeleze kuchukizwa kwao na vitendo vya utawala bandia wa Israel na kutangaza uungaji mkono wao kwa watu wanaodhulumiwa wa Palestina.
Ujumbe huo pia umesema: "Kuuawa kwa watu wa Afghanistan, haswa Waislamu wa madhehebu ya Shia, katika hujuma ya hivi karibuni, ni tukio chungu sana ambalo linapaswa kulaaniwa."
Milipuko mitatu ya mabomu iliyotokea siku ya Jumanne iliyopita mbele ya shule ya wavulana katika kitongoji cha Mashia wa Hazara kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul iliua takriban watu sita na kujeruhi wengine 24.