Khatibzadeh: Mapumziko ya muda mrefu si kwa maslahi ya mazungumzo ya Vienna
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i82912-khatibzadeh_mapumziko_ya_muda_mrefu_si_kwa_maslahi_ya_mazungumzo_ya_vienna
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa: Iran na Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuwa mapumziko ya muda mrefu si kwa maslahi ya mazungumzo ya Vienna.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 25, 2022 07:00 UTC
  • Khatibzadeh: Mapumziko ya muda mrefu si kwa maslahi ya mazungumzo ya Vienna

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa: Iran na Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuwa mapumziko ya muda mrefu si kwa maslahi ya mazungumzo ya Vienna.

Saeed Khatibzadeh leo Jumatatu amezungumza na waandishi wa habari hapa Tehran na kueleza kuwa kwenda mapumziko ya muda mrefu si kwa maslahi ya mazungumzo ya Vienna na kwamba ni vyema mapumziko hayo yapelekee kukutana ana kwa ana pande husika haraka iwezekanavyo. Amesema suala hilo liko katika ajenda ya kazi.  

Kuhusu kuhamishwa sentrifyuji (mashinepewa), Khatibzadeh amebainisha kuwa: Iran ni nchi mwanachama iliyosaini mkataba wa NPT na kuafiki mkataba huo unaopiga marufu uenezaji na usambazaji wa silaha za nyuklia. Amesema, Wakala wa IAEA ulipewa taarifa kuhusu kuhamishiwa sentrifyuji hizo huko Natanz katika eneo salama baada ya kamera kuharibiwa katika eneo la awali. 

Mashinepewa zilizohamishiwa katika taasisi ya Natanz 

Kuhusu mazungumzo kati ya Rais Joe Biden wa Marekani na Naftali Bennet Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Serikali ya Biden tangu siku ya kwanza ilifanya kila ilichoweza kuhakikisha kuwa fursa zote za kidiplomasia zinapotea; suala linaloonyesha namna White House ilivyochanganyikiwa kwa yale inayodai kuwa inayafuatilia huko Vienna.  

Amesema, kile kinachojiri sasa kati ya Iran na Marekani ni makabiliano ya kimitazamo kati ya pande mbili; huku mtazamo wa upande mmoja ukipuuza haki za kimataifa na kujaribu kutwisha sera zake kwa masuala yote ya kimataifa. Iran inaamini kuwa mazungumzo ambayo yamesainiwa yamefungwa, na yanapaswa kuheshimiwa.