Iran inaongoza eneo katika kuangamiza Malaria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i82942-iran_inaongoza_eneo_katika_kuangamiza_malaria
Mkurugenzi wa Kituo cha Magonjwa ya Kuambukiza katika Wizara ya Afya ya Iran amesema Iran ndiyo nchi iliyofanikiwa zaidi katika kuangamiza malaria katika ukanda wa Mediteranea Mashariki.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Apr 26, 2022 06:32 UTC
  • Iran inaongoza eneo katika kuangamiza Malaria

Mkurugenzi wa Kituo cha Magonjwa ya Kuambukiza katika Wizara ya Afya ya Iran amesema Iran ndiyo nchi iliyofanikiwa zaidi katika kuangamiza malaria katika ukanda wa Mediteranea Mashariki.

Kwa mujibu wa wa Shirika la Afya Duniani (WHO), nchi za Ukanda wa Mediteranea Mashariki (EMRO), ni Afghanistan, Bahrain, Djibouti, Misri, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Iraq, Jordan, Kuwait, Lebanon, Libya, Morocco, Palestina, Oman, Pakistan, Qatar, Saudi Arabia, Somalia, Sudan, Syria, Tunisia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Yemen.

Akizungumza Jumanne, Mohammad Mahdi Gouya, Mkuu wa Kituo cha Magonjwa ya Kuambukiza katika Wizara ya Afya ya Iran amesema hakuna nchi ya eneo hilo yenye upana na idadi ya watu kama Iran iliyofanikiwa kuangamiza Malaria na kuongeza kuwa, kuangamiza Malaria ni kati ya malengo saba ya ustawi endelevu ya Iran.

Mahdi Gouya ameongeza kuwa, Iran imepokea cheti cha kuangamiza malaria kutoka kwa Shirika la Afya Duniani. Amesema mafanikio hayo ni makubwa kiafya na pia ni muhimu kiujumla katika ustawi wa Iran.

Ameongeza kuwa, kutokana na jitihada kubwa za wafanyakazi wa sekta ya afya, katika kipindi cha miaka mitatu sasa hakujaripotiwa kesi yoyote ya malaria nchini Iran. 

Jana Aprili 25 ilikuwa ni siku ya kimataifa ya kutokomeza ugonjwa wa malaria duniani. Mkakati wa kimataifa wa malaria wa WHO unatoa wito wa kupunguzwa kwa asilimia 90 kwa visa na vifo duniani kote ifikapo mwaka 2030, lengo ambalo linahitaji uwekezaji wa haraka ili kubaini na kupeleka ubunifu muhimu wa kupambana na janga hilo kwa lengo la kulinda watu kila mahali dhidi ya malaria.