Spika Qalibaf: Kuunga mkono Palestina na Quds ni kipaumbele cha Iran
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuunga mkono Palestina na Quds ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele na taifa hili la Kiislamu.
Muhammad Baqer Qalibaf amesema hayo leo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Khalil al-Hayya, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na kusisitiza kwamba, damu ya mashahidi ni dhamana ya ushindi Palestina.
Dakta Qalibaf amesema pia kuwa, suala la Quds na Palestina lina mizizi mirefu nchini Iran na kwamba, Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikuwa akiitambua kadhia ya Palestina kuwa jambo muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu na ndio maana akaichagua na kuitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua na hujuma za utawala haramu wa Israel na uistikbari wa dunia pamoja na hatua za baadhi ya mataifa ya Kiarabu za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu na kusema kuwa, umma wa Kiislamu, makundi ya muqawama na ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla unapaswa kupandisha gharama za kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel.
Kwa upande wake, Khalil al-Hayya, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema, Wazayuni wanafanya njama za kuwafukuza wakazi wa asili kutoka katika Msikiti wa al-Aqswa na badala yake wawaweke Wazayuni.