Iran yajiundia meli mbili mpya za kivita
Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran linatazamiwa kupokea meli mbili za kivita ambazo zimeundwa kikamilifu hapa nchini.
Hayo yamedokezwa na Admeri Shahram Irani, Kamanda wa Jeshi la Majini la Iran ambaye amesema meli hizo mbili za kivita zilizoundwa nchini zimepewa majina ya Zagro na Damavand-2 na kuongeza kuwa zitaanza kutumika hivi karibuni.
Katika mahojiano na Televisheni ya IRINN, Admeri Irani amesema manowari hizo mbili za kisasa zitakabidhiwa Jeshi la Majini la Iran katika sherehe maalumu. Ameongeza kuwa hivi sasa manowari hizo zinafanyiwa majaribio ya mwisho huku maafisa wanaotazamiwa kuzitumia wakipata mafunzo hasa kwa kuzingatia kuwa zimeundwa kwa teknolojia za kisasa kabisa.
Aidha kamanda huyo amesema hivi sasa Iran imepiga hatua kubwa katika kuunda meli za kivita zenye uwezo wa kufika maeneo yote katika bahari za dunia na kuongeza kuwa uzalishaji kwa wingi wa meli hizo utaanza hivi karibuni.
Admeri Irani amesema kile ambacho kinaifanya Marekani ichukizwe na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa nchi hii inamiliki teknolojia ya kujiundia meli za kivita na nyambizi sambamba na kuzitumia katika maji ya kimataifa. Hali kadhalika amesema harakati za majeshi ya majini ya Iran zinafanyika katika fremu ya kujihami na diplomasia ya baharini huku akisisitiza kuwa usalama wa eneo unapaswa kudhaminiwa na nchi za eneo.
Katika miaka ya hivi karibuni Iran imeweza kupiga hatua kubwa za kujitosheleza katika sekta ya kijeshi ambapo inajiundia zana za kijeshi na kivita kwa teknolojia ya kisasa kabisa.
Iran inasisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua za kuimarisha uwezo wake wa kijeshi ukiwemo uwezo wa makombora kwa lengo la kujihami.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran amekuwa akisisitiza umuhimu wa Iran kujiimarisha katika sekta ya ulinzi huku akiwakosoa maadui wanaopinga mpango wa makombora ya kujihami ya nchi hii.