Iran yazidi kuimarisha biashara na nchi za Afrika
Naibu mkuu wa Shirika la Kukuza Biashara la Iran (TPO) anayeshughulikia maendeleo ya masoko ya nje amesema shirika lake linatafuta njia za kutekeleza mifumo ya biashara ya kubadilishana bidhaa na washirika wa kibiashara wa bara la Afrika.
"Kwa kuzingatia utekelezaji wa utaratibu wa biashara ya kubadilishana bidhaa na Shirika la Kukuza Biashara na nchi kadhaa, tunatumai kufaidika na jukwaa hili na washirika wa kibiashara wa Kiafrika pia," Ahmad-Reza Alaei Tabatabaei alisema.
Afisa huyo alibainisha kuwa TPO imetayarisha orodha ya bidhaa 1,100 ambazo zinaweza kujumuishwa katika biashara ya kubadilishana bidhaa na nchi za Afrika.
Ikirejelea mipango ya TPO ya kupanua biashara na Afrika, Tabatabaei ilitangaza uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji na uimarishaji wa uwepo wa waambata wa kibiashara wa Iran katika bara hilo. Kwa mujibu wa afisa huyo, changamoto muhimu zaidi kwa wafanyabiashara wa Iran kuhusiana na bara la Afrika ni ukosefu wa maarifa na ujuzi wa masoko yake.
Aidha alibainisha kuwa changamoto nyingine muhimu katika kupanua wigo wa biashara na nchi za Afrika ni usafiri na usafirishaji, hasa haja ya kuendeleza miundombinu ya usafiri wa baharini.
Akizungumzia uwezo mkubwa wa Iran katika uga wa huduma za kiufundi na uhandisi amesema: "Nchi za Afrika ni miongoni mwa waagizaji muhimu wa huduma za kiufundi na uhandisi duniani, na kwa bahati nzuri Iran imeendelea zaidi katika eneo hili katika miaka ya hivi karibuni."
Afisa huyo pia aliashiria ongezeko la asilimia 45 la mauzo ya bidhaa za Iran barani Afrika, akisema: "Kwa sasa, Ghana ni kituo cha kwanza cha mauzo ya Iran barani Afrika, ikifuatiwa na Afrika Kusini na Nigeria katika nafasi za pili na tatu."