Iran: Tumeitaarifu IAEA kuhusu shughuli zetu katika kituo cha nyuklia cha Natanz
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i84886-iran_tumeitaarifu_iaea_kuhusu_shughuli_zetu_katika_kituo_cha_nyuklia_cha_natanz
Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema Jamhuri ya Kiislamu imelitaarifu Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kuhusu mpango wake wa kuhamishia mji wa Natanz katikati ya Iran, shughuli za kituo cha nyuklia cha TESA kilichoko katika mji wa Karaj, viungani mwa mji mkuu Tehran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 18, 2022 08:02 UTC
  • Iran: Tumeitaarifu IAEA kuhusu shughuli zetu katika kituo cha nyuklia cha Natanz

Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema Jamhuri ya Kiislamu imelitaarifu Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kuhusu mpango wake wa kuhamishia mji wa Natanz katikati ya Iran, shughuli za kituo cha nyuklia cha TESA kilichoko katika mji wa Karaj, viungani mwa mji mkuu Tehran.

Behrouz Kamalvandi amesema hayo katika mahojiano na shirika la Nour News na kufafanua kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imechukua hatua hiyo licha ya kuwa haikulazimika kufanya hivyo, kwa lengo la kuimarisha usalama katika vituo vyake vyote vya nyuklia.

Ameashiria shambulio dhidi ya kituo cha TESA mwaka jana na kueleza kuwa, Iran imeamua kuhamishia baadhi ya shughuli za kituo hicho hadi katika kituo cha Natanz, ili kuzuia kujikariri hujuma za namna hiyo.

Juni mwaka jana, kituo hicho cha nyuklia kilichoko Karaj kilihujumiwa katika shambulio ambalo linalaumiwa utawala wa Kizayuni wa Israel, ambapo kamera za ukaguzi katika kituo hicho ziliharibiwa.

Kituo cha nyuklia cha Natanza

Akizungumza na waandishi wa habari pambizoni mwa safari yake ya katika mji wa Natanz mkoani Esfahan hivi karibuni, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, Mohammad Eslami alisema, katika muda wa miongo miwili iliyopita, yamefanyika mazungumzo mengi kati ya Iran na nchi za Magharibi kuhusiana na shughuli za nyuklia za Iran zinazofanyika kwa malengo ya amani, na umefanyika ukaguzi mkubwa na wa mara chungu nzima mpaka hatimaye yakafikiwa makubaliano ya JCPOA .

Alisisitiza kuwa, kutokana na ukaguzi uliofanywa, iliafikiwa kuwa faili la tuhuma zilizoibuliwa dhidi ya Iran katika kalibu ya PMD (uwezekano wa mpango wa nyuklia wa Iran kuwa na malengo ya kijeshi) lifungwe.