Matetemeko ya ardhi yaua watu 5 kusini mwa Iran, makumi wajeruhiwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i85406-matetemeko_ya_ardhi_yaua_watu_5_kusini_mwa_iran_makumi_wajeruhiwa
Matetemeko kadhaa ya ardhi yaliyotokea kwa kufuatana katika mkoa wa Hormozgan huko kusini mwa Iran yakiwa na zaidi ya daraja 6 kwa kipimo cha Richter yamesababisha vifo vya watu 5 na kujeruhi wengine 39.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Jul 02, 2022 03:43 UTC
  • Matetemeko ya ardhi yaua watu 5 kusini mwa Iran, makumi wajeruhiwa

Matetemeko kadhaa ya ardhi yaliyotokea kwa kufuatana katika mkoa wa Hormozgan huko kusini mwa Iran yakiwa na zaidi ya daraja 6 kwa kipimo cha Richter yamesababisha vifo vya watu 5 na kujeruhi wengine 39.

Idara ya Taifa inayoshughulikia tetemeko la ardhi imetangaza kuwa tetemeko la ardhi lililokuwa na 6.1 kwa kipimo cha Rishta limetokea katika kina cha kilomita kumi chini ya ardhi katika maeneo ya Bandar Khamir na Bandar Lengeh katika mkoa wa Hormozagan huko kusini mwa Iran na kufuatiwa na tetemeko jingine lililokuwa na 6.1 katika kina cha kilomita 27 chini ya ardhi kandokando ya eneo la Bandar Kong mapema leo Jumamosi. 

Tetemeko jingine la tatu lililokuwa na 6.3 kwa kipimo cha Rishta limetokea katika eneo la Bandar Khamir. 

Kwa mujibu wa takwimu rasmi, matetemeko makubwa ya ardhi yaliyotokea magharibi mwa mkoa wa Hormozgan hadi sasa yamesababisha vifo vya watu 5 na kujeruhiwa wengine 39 katika kijiji cha Sayeh Khosh cha Bandar Lengeh.

Hormosgan, Iran

Matetemeko hayo ya ardhi yalikuwa na nguvu kubwa kiasi kwamba yamesikika pia huko Bandar Abbas na katika miji mingine ya mkoa wa Hormozgan, visiwa vya Ghuba ya Uajemi na hata katika nchi za Kiarabu za kandokando ya Ghuba ya Uajemi.

Waziri wa Afya, Tiba na Elimu ya Udaktari wa Iran  Bahram Ainullahi ametoa wito wa kushughulikiwa haraka waathiriwa na mitetemeko hiyo ya ardhi na kuwa tayari kwa hospitali za mkoa wa Hormozgan na kwa ajili ya kupokea majeruhi wa mitetemeko hiyo.