Gharibabadi :Marekani haina ustahiki wa kuzungumzia haki za binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i85480-gharibabadi_marekani_haina_ustahiki_wa_kuzungumzia_haki_za_binadamu
Afisa mwandamizi wa haki za binadamu nchini Iran amesema Marekani haina ustahiki wa kuzungumzia suala la haki za binadamu kutokana na namna inavyokiuka kwa wingi haki za binadmau duniani.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Jul 04, 2022 03:21 UTC
  • Gharibabadi :Marekani haina ustahiki wa kuzungumzia haki za binadamu

Afisa mwandamizi wa haki za binadamu nchini Iran amesema Marekani haina ustahiki wa kuzungumzia suala la haki za binadamu kutokana na namna inavyokiuka kwa wingi haki za binadmau duniani.

Katibu wa Baraza Kuu la Haki za Kibinadamu la Iran Kazem Gharibabadi amesisitiza kuwa Marekani, kwa vyovyote vile, haina sifa ya kuzungumzia suala la haki za binadamu.

Afisa huyo ametoa tamko hilo akizungumza katika Kongamano la Nne la Kimataifa la Haki za Binadamu za Kimarekani kwa Mtazamo wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei.

Gharibabadi ameongeza kuwa, "Marekani inapaswa kuwajibishwa kuhusu watu wanaokandamizwa, ambao wamepoteza maisha kutokana na ugaidi, vikwazo, uchokozi na uvamizi,"

Ametoa mfano wa watu wa Yemen ambao wanakabiliwa vita vinavyoongozwa na Saudi Arabia na washirika wake, vita ambavyo vinaungwa mkono na Marekani. Wayemeni bado wananyimwa msaada wa kimsingi zaidi wa kibinadamu kutokana na wavamizi na waaungaji mkono wao ambao wana "tabia ya ubeberu na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu," afisa huyo amebainisha.

Akihutubia mkutano huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran katika Masuala ya Kisiasa, Ali Baqeri-Kani amesema kukanyaga haki za binadamu za watu huru ni "sehemu" ya sera ya nje ya Marekani.

Watoto wa Yemen ni waathirika wakuu wa vita vya Saudia dhidi ya Yemen ambavyo vinaungwa mkono kikamilifu na Marekani

Amesema, "Mtu anaweza kusema kwa ujasiri kwamba hakuna taifa lolote katika dunia ya leo ambalo halijaonja ladha chungu ya haki za binadamu kwa mtazamo wa Marekani."

‘Baqeri-Kani amesema "vikwazo na ugaidi" ni nguzo kuu za haki za binadamu za Kimarekani na kuongeza, "Ikiwa watanyang'anywa nguzo hizi mbili, wanaweza wasiweze kuendelea na satwa yao ya kibeberu na njama dhidi ya wengine.

Katika kalenda ya Iran tarehe 27 Juni hadi tatu Julai hutambuliwa kama Wiki ya Haki za Binadamu za Kimarekani ambapo katika wiki hii utambulisho halisi wa jinai za Marekani hubainishwa wazi mbele ya walimwengu na hivyo kufichua hadaa ya Marekani katika madai yake kuwa eti ni mtetezi wa haki za binadamu. Katika wiki hii pia huangaziwa zaidi jinai za Marekani dhidi ya Wairani wasio na hatia.