Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alaani mauajii ya Shinzo Abe
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i85636-waziri_wa_mambo_ya_nje_wa_iran_alaani_mauajii_ya_shinzo_abe
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani mauaji ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, ambaye alifariki baada ya kupigwa risasi akiwa katika kampeni za uchaguzi wa bunge.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 08, 2022 23:10 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alaani mauajii ya Shinzo Abe

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani mauaji ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, ambaye alifariki baada ya kupigwa risasi akiwa katika kampeni za uchaguzi wa bunge.

Katika ujumbe aliotuma kwa lugha za Kifarsi na Kijapani kwenye akaunti yake ya Twitter siku ya Ijumaa, Hossein Amir-Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametuma salamu za rambirambi kwa watu na serikali ya Japan kufuatia mauaji ya Abe.
"Huduma zake za thamani kama mwanasiasa mashuhuri, zikiwemo [zile ambazo zililenga] kuendeleza uhusiano kati ya mataifa mawili ya Iran na Japan, hazitasahaulika," Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika katika Twitter.

Abe mwenye umri wa miaka 67, kiongozi wa muda mrefu zaidi wa Japan, alikuwa akitoa hotuba  karibu na kituo cha treni katika mji wa magharibi wa Nara wakati alipopigwa risasi na mshambuliaji siku ya Ijumaa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kan'ani  naye pia amelaani mauaji ya Shinzo Abe kwa kusema: "Iran Kama nchi iliyoathiriwa na ugaidi na ambayo imepoteza viongozi wakubwa kwa hujuma za magaidi, tunafuatilia habari za mauaji ya waziri mkuu wa zamani wa Japan, Shinzo Abe kwa wasiwasi."

Ujumbe wa Twitter wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kufuatia mauaji ya Shinzo Abe

Mtu mmoja anayeaminika kuwa ndiye aliyempiga risasi Abe tayari ameshatiwa mbaroni. Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Japan, Shinzo Abe aliyekuwa na umri wa miaka 67 alizimia mara tu baada ya kushambuliwa na alionekana akivuja damu, kabla ya kupelekwa haraka hospitali ambako alifariki.

Shirika la habari la Japan NHK limemnukuu mtuhumiwa huyo Tetsuya Yamagami akiwaambia polisi kwamba alidhamiria kumuua Waziri Mkuu wa zamani Shinzo Abe kwa sababu hakuridhika naye.

Abe alikuwa waziri mkuu wa Japan aliyekaa uongozini kwa muda mrefu zaidi kutoka mwaka 2006 hadi mwaka 2020.