Amir Abdollahian: Makampuni ya Italia yana shauku ya kuwekeza nchini Iran
Hossein Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema amefurahishwa na kiwango cha utayari wa makampuni ya Italia wa kushirikiana na Iran, na kusisitiza haja ya kurejeshwa safari za moja kwa moja za ndege kati ya nchi mbili hizi.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesema mapema leo Jumatano katika ujumbe wake wa Twitter kwamba: "Kwa mwaliko wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia na Iran, nikiwa mjini Roma jana Jumanne, ambapo nilikutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa makampuni ya sekta binafsi ya Italia. Hamu yao ya kufanya kazi na Iran ilikuwa ya kuvutia sana. Kurejeshwa safari za moja kwa moja za ndege kati ya Tehran na Rome ni muhimu kwa juhudi zetu za pamoja katika uwanja huo."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mikutano ya ngazi za juu akiwa nchini Italia na Vatican.
Amir Abdollahian alikuwa tayari ameelezea mazungumzo yake ya Jumatatu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia na pia mikutano yake na wawakilishi wa sekta binafsi ya Italia, wafanyabiashara na wawekezaji kuwa chanya na yenye kuzaa matunda.
Ameongeza kuwa masuala aliyozungumza na waziri mwenzake wa Italia ni pamoja na kuimarisha diplomasia ya bunge kwa kuzingatia itifaki zilizotiwa saini mwaka 2000 kuhusu ushirikiano wa mabunge ya nchi hizi mbili.