Rais Raisi: Iran ya Kiislamu inazidi kupata nguvu zaidi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Iran ya Kiislamu leo ina nguvu zaidi ya wakati wowote ule.
Akizungumza Alhamisi katika mkoa wa Kermanshah, Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema uingiliaji wa Marekani na waitifaki wake katika eneo ni chanzo cha ukosefu wa usalama. Ameongeza kuwa, mataifa ya Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi yanachukia sana uhusiano wa kidhalilishaji na Marekani pamoja na waitifaki wake.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema utawala wa Kizayuni wa Israel unapaswa kufahamu kuwa, haupaswi kuwa na macho ya tamaa na kuongeza kuwa, Marekani na waitifaki wake wafahamu kuwa taifa adhimu la Iran katu halitakubali kuona eneo hili likiwa katika mgogoro na ukosefu wa usalama.
Juzi pia Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza bayana kuwa, Iran haiataachana na misimamo yake ya haki na ya kimantiki na hakuna aliye na haki ya kutumia lugha ya mabavu mkabala wa taifa la Iran.

Akijibu madai ya karibuni ya Marekani kuhusu mapatano ya JCPOA, Rais Raisi alieleza kuwa: Wamarekani wamesema Iran inapaswa kurejea katika mapatano hayo ilhali Jamhuri ya Kiislamu haijawahi kujitoa katika JCPOA, bali ni Marekani iliyokiuka makubaliano hayo."
Akiashiria safari ya Rais Biden wa Marekani katika eneo, Rais wa Iran alisema: "Iwapo ziara za viongozi wa Marekani katika nchi za eneo hili ni za kutaka kuimarisha nafasi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kuanzisha uhusiano baina ya utawala huo na baadhi ya nchi, basi juhudi zao hazitawadhaminia usalama Wazayuni kwa njia yoyote ile."