Iran yalamikia rasmi hatua ya Uswidi ya kumfunga Muirani kwa tuhuma bandia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i85892-iran_yalamikia_rasmi_hatua_ya_uswidi_ya_kumfunga_muirani_kwa_tuhuma_bandia
Iran imemuita balozi mdogo wa Uswidi mjini Tehran na kumkabidhi malalamiko ya kupinga hukumu ya mahakama ya Uswidi dhidi ya raia wa Iran ambaye amefungwa kifungo cha maisha jela kutokana na tuhuma zisizo na msingi zilizotolewa dhidi yake na kundi la kigaidi la MKO linaloipinga Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 15, 2022 02:41 UTC
  • Iran yalamikia rasmi hatua ya Uswidi ya kumfunga Muirani kwa tuhuma bandia

Iran imemuita balozi mdogo wa Uswidi mjini Tehran na kumkabidhi malalamiko ya kupinga hukumu ya mahakama ya Uswidi dhidi ya raia wa Iran ambaye amefungwa kifungo cha maisha jela kutokana na tuhuma zisizo na msingi zilizotolewa dhidi yake na kundi la kigaidi la MKO linaloipinga Iran.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Tatu cha Ulaya Magharibi cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alimuita balozi mdogo wa Uswidi siku ya Alkhamisi baada ya mahakama ya nchi hiyo kutoa hukumu dhidi ya Hamid Nouri, afisa wa zamani wa mahakama ya Iran kwa msingi wa tuhuma za kundi la kigaidi la MKO.

Mwanadiplomasia huyo wa Uswidi alipewa barua rasmi ya Iran ya kupinga hukumu hiyo.

Afisa huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ameitaja hukumu hiyo kuwa "kinyume cha sheria na kinyume cha kanuni za kimataifa." Aidha ameitaja  mahakama hiyo kuwa "isiyo na ujuzi" na kesi hiyo kuwa iliyo "kinyume cha sheria."

Aidha amesema Nouri amehukumiwa kutokana na "ushahidi usio na mashiko" wa wanachama wa kundi la kigaidi la MKO. Amebaini kuwa kundi hilo limewaua Wairani 17,000 wasio na hatia.

Hali kadhalika ameikosoa Stockholm kwa "mtazamo wake wa upendeleo kuhusu ugaidi" kwa kutegemea madai ya kundi la kigaidi la MKO dhidi ya Nouri.

Infaa kuashirikia hapa kuwa Hamid Nouri amehukumiwa kifungo cha juu kabisa cha maisha gerezani kwa tuhuma kuwa afisa huyo wa zamani wa Idara ya Mahakama ya Iran alihusika katika utesaji wa wafungwa mwaka 1988. Hata hivyo Nouri amekanusha kabisa tuhuma hizo.

Mnamo Novemba 9 mwaka 2019, Hamid Nouri alielekea Sweden kwa lengo la kutatua hitilaifu za kifamilia za binti yake na punde baada ya kuwasili alikamatwa na maafisa wa usalama wa nchi hiyo na amekuwa akishikiliwa gerezani kwa muda wa karibu miezi 30.

Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Stockholm iliyosikiliza kesi ya Nouri

Afisa huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekumbusha zaidi kwamba, raia huyo wa Iran alifungwa katika seli ya upweke na vile vile kuwekewa  vikwazo na mashinikizo mengine mbalimbali ya kiakili na kimwili, na kusema unyama huo ni dhihirisho la kivitendo la mateso na ukiukwaji wa haki za kimsingi za binadamu.

Amesema serikali ya Uswidi ndiyo inayohusika na ukiukwaji wa haki za raia wa Iran na jambo hilo litaathiri vibaya uhusiano wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kiislamu.

Afisa huyo ametoa wito kwa Stockholm kubatilisha hukumu ya Nouri, kuwezesha kuachiliwa kwake mara moja, na kufidia hali mbaya ambayo ametwishwa.

Balozi mdogo wa Uswidi mjini Tehran  amesema raia huyo wa Iran atapewa nafasi ya kukata rufaa dhidi ya hukumu aliyopewa, na amesema ataifikishia serikali yake malalamiko ya Iran.