Iran yakanusha madai ya Marekani kuwa imeipa Russia droni za kivita
Iran imesema Marekani inafuatilia "malengo mahususi ya kisiasa" kwa kudai kwamba Tehran inapanga kuikabidhi Russia mamia ya droni au ndege zisizo na rubani zenye uwezo wa kusheheni silaha za kivita.
Katika mazungumzo ya simu ya Ijumaa na mwenzake wa Ukraine Dmytro Kuleba, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian alitupilia mbali shutuma za hivi majuzi zilizotolewa na mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani dhidi ya Tehran. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema madai kama hayo - sanjari na ziara ya Rais wa Marekani Joe Biden katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu (Israel) - yanaambatana na malengo fulani maalum ya kisiasa ambayo White House inayafuatilia.
Mnamo Julai 11, Jake Sullivan alidai kuwa Washington ilipokea "taarifa" zinazoonyesha kwamba Iran ilikuwa inajiandaa kuipatia Russia "mamia ya droni , ikiwa ni pamoja na droni zenye uwezo wa kusheheni silaha na mpango huo unapangwa kutekelezwa haraka" kwa ajili ya matumizi katika vita vinavyoendelea nchini Ukraine.
Tangu kuanza kwa "operesheni maalum ya kijeshi" ya Russia nchini Ukraine mnamo Februari 24, Marekani na washirika wake wa Ulaya wamekuwa wakiipa Kiev silaha za kisasa, pamoja na mifumo ya makombora, ili kupambana na Jeshi la Russia.
Kwingineko katika mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alimwambia waziri mwenzake wa Ukraine kwamba msimamo wa kimsingi wa Tehran ni kupinga vita duniani kote.
Amesema Iran itaendelea kufanya kazi kusaidia kumaliza mzozo kati ya Russia na Ukraine. "Kama tulivyotangaza tangu mwanzo wa mgogoro [huko Ukraine], tunapinga vita nchini Afghanistan, Yemen, Palestina na Ukraine," Amir-Abdollahian alisema.
"Msimamo wa kimsingi na bayana wa Jamhuri ya Kiislamu ni kupinga vita sambamba na kuunga mkono jitihada za kukomoesha vita. Msimamo huo ni kinyume na msimamo wa baadhi ya nchi za Magharibi, ambazo zinafuata sera za undumakuwili."
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesema Tehran iko tayari kupanua uhusiano na Ukraine katika nyanja zote hususan katika sekta ya uchumi na kilimo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine naye amepongeza msimamo wa Iran dhidi ya vita na juhudi zake za kusaidia kusimamisha mapigano au kutafuta suluhu ya kisiasa kwa mgogoro unaoendelea.
Kuleba alisema Ukraine ilikuwa tayari kufungua ukurasa mpya katika uhusiano na Tehran. Amesema Iran na Ukraine hazipaswi kuruhusu wengine kuvuruga uhusiano wao kupitia shutuma.