Kan’ani: Matamshi ya Biden kuhusu Iran yanalenga kuendeleza fitina za Washington
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i85962-kan’ani_matamshi_ya_biden_kuhusu_iran_yanalenga_kuendeleza_fitina_za_washington
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema baadhi ya madai na tuhuma zinazotolewa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa safari ya Rais Joe Biden wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, ikiwa ni pamoja na matamshi yake akiwa Jeddah si za kweli na hazina msingi wowote.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Jul 17, 2022 03:33 UTC
  • Kan’ani: Matamshi ya Biden kuhusu Iran yanalenga kuendeleza fitina za Washington

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema baadhi ya madai na tuhuma zinazotolewa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa safari ya Rais Joe Biden wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, ikiwa ni pamoja na matamshi yake akiwa Jeddah si za kweli na hazina msingi wowote.

Nasser Kan'ani Chafi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameendelea kusema kuwa: "Madai haya ya uwongo yanaambatana na sera ya uchochezi na ya kuleta mvutano  inayofuatiliwa na Washington katika eneo hilo."

Aidha amesema Marekani imeweka historia kama nchi ya kwanza iliyowahi kutumia bomu la atomiki duniani sambamba na uingiliaji wake katika masuala ya ndani ya nchi za eneo, kukalia kwa mabavu na kuvamia kijeshi nchi mbali mbali, kuuza idadi kubwa ya silaha angamizi na kuhimiza chokochoko za kijeshi katika eneo. Ameongeza kuwa: "Marekani kwa mara nyingine inafuatilia sera zilizofeli za chuki dhidi ya Iran kwa lengo la kuibua taharuki na migogoro katika eneo."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran hali kadhalika ameashiria namna ambavyo Marekani imekuwa ikunga mkono bila masharti utawala wa Kizayuni wa Israel ambao unakalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kuongeza kuwa: "Bila shaka, serikali ya Marekani ndiyo mshirika mkuu katika kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina na mji mtakatifu wa Kipalestina, jinai na ukatili wa kila siku wa utawala huo dhidi ya Wapalestina na utawala wa kibaguzi  au apathaidi, na ukiukaji wa kimfumo wa haki za binadamu za Wapalestina wanaodhulumiwa na wanaopambana."

Mkutano wa Biden na Mfalme wa Saudia

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesisitiza kuwa siasa za kistratijia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika utumiaji wa teknolojia ya amani ya nyuklia ndani ya fremu ya sheria na kanuni za kimataifa na kufungamana na kuendelea mazungumzo ya kuondoa vikwazo na kuongeza kuwa: "Shutuma za Marekani kuhusiana na mpango wa amani wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kufumbia kwake macho miongo kadhaa ya hadaa ya utawala wa Kizayuni ambao ni utawala usiokuwa mwanachama katika Mkataba wa Kuzuia Uenezaji silaha za nyuklia na mmiliki mkubwa zaidi wa silaha za nyuklia katika eneo ni ishara kubwa ya udanganyifu na unafiki wa serikali ya Marekani."

Mwishoni msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesisitiza juu ya sera ya msingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kukaribisha mazungumzo na majirani zake na ubunifu wa ndani ya eneo na kuongeza kuwa: "Inatarajiwa kuwa serikali za eneo zitaitikia mwaliko na mipango ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya mazungumzo na ushirikiano wa kieneo, kuchukua hatua zenye manufaa kwa usalama wa pamoja, amani na utulivu na maendeleo ya pamoja."