Iran karibuni itakuwa kitovu cha kurushia satalaiti katika eneo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i85964-iran_karibuni_itakuwa_kitovu_cha_kurushia_satalaiti_katika_eneo
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Iran ametangaza kuwa Jamhuri ya Kiislamu imekuwa nguzo ya kurushia satalaiti katika eneo.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Jul 17, 2022 03:37 UTC
  • Iran karibuni itakuwa kitovu cha kurushia satalaiti katika eneo

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Iran ametangaza kuwa Jamhuri ya Kiislamu imekuwa nguzo ya kurushia satalaiti katika eneo.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepiga hatua muhimu katika urushaji wa satelaiti kutokana na kujikita zaidi katika kuunda maroketi ya kubeba satelaiti na kwa msingi huo imeendeleza sekta ya kurusha satelaiti katika anga za mbali sambamba na kujitegenezea satelaiti.
Sasa, wataalamu wa Iran wamefanikiwa kukamilisha mzunguko kamili wa teknolojia ya anga za juu, yaani ujuzi wa msingi wa kituo cha nchi kavu cha kurushia satalaiti,  maroketi ya kurusha sataliti na kituo cha kupokea data za satelaiti zilizo katika anga mbali.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRIB, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Iran, Isa Zarepour, amesema kuwa Iran karibuni itakuwa mojawapo ya vituo vikuu vya kurushia satelaiti anga za mbali zilizo katika  umbali wa kilomita 500 kutoka ardhini ambalo kitaalamu linajulikana kama LEO. Amesema Iran sasa inaweza kutoa huduma kwa nchi zingine katika uga wa kurusha satalaiti katika eneo hilo la anga za juu.

Zarepour ameongeza kuwa, miundombinu ya anga za juu ya Iran inaendelezwa na hivi sasa  nchi hii imeweza kufanikiwa katika sekta za kuanzia ujenzi wa satelaiti na maroketi ya kuruhsia satelaiti hadi vituo vya kupokea data za satalaiti zilizo katika anga za juu. 

Satalaiti ya kijeshi ya Iran ijulikanayo kama Nour-1 iliyorushwa katika anga za mbali mwaka 2020 kwa mafanikio 

Katika miongo minne iliyopita, Iran imepiga hatua endelevu na za kimaendeleo katika uga wa kufikia teknolojia ya anga za juu.
Ijapokuwa maadui wamejaribu kuzuia maendeleo ya kiuchumi na kisayansi ikiwemo sekta ya anga ya juu ya Iran kwa vikwazo vya kila namna, lakini licha ya vikwazo na mashinikizo hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata mafanikio mbalimbali ya teknolojia ya anga na anga za mbali. 

Tofauti kati ya mpango wa anga ya juu wa Iran na nchi nyingine za eneo la Magharibi mwa Asia ni kwamba Iran imeegemea kwenye uwezo wake wa ndani na imenufaika na teknolojia yake ya ndani.