Rais Putin wa Russia anawasili Tehran leo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i86030-rais_putin_wa_russia_anawasili_tehran_leo
Rais Vladimir Putin wa Russia leo Jumanne anawasili Tehran, mji mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa lengo la kushiriki katika kikao cha pande tatu baina ya Russia, Iran na Uturuki.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 18, 2022 23:18 UTC
  • Rais Putin wa Russia anawasili Tehran leo

Rais Vladimir Putin wa Russia leo Jumanne anawasili Tehran, mji mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa lengo la kushiriki katika kikao cha pande tatu baina ya Russia, Iran na Uturuki.

Dmitry Peskov Msemaji wa Ikulu ya Kremlin ameeleza kuwa, Rais Vladmir Putin Jumanne ya leo Julai 19 atafanya safari mjini Tehran kwa lengo la kushiriki katika mkutano wa pande tatu wa Marais  wa Iran, Russia na Uturuki katika fremu ya Mazungumzo ya Astana kuhusiana na mchakato wa amani ya Syria. 

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki tayari yuko mjini Tehran kwa ajili ya kushiriki katika kikao hicho ambacho mwenyeji wake ni Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Iran.

Balozi wa Russia nchini Iran Levan Dzhagaryan ameiambia televisheni ya Rossiya-24  kwamba, akiwa mjini Tehran, Rais Putin pia anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Marais Erdogan wa Uturuki, Putin wa Russia na Raisi wa Iran

Naye Mohammad Farazmand  balozi wa Iran mjini Ankara Uturuki ameandika hivi karibuni  katika ukurasa wake wa Twitter kuwa wakati wa safari ya Erdogan mjini Tehran, "Kutafanyika vikao viwili muhimu mjini Tehran. Kwanza ni kikao cha Kamati Kuu ya Uhusiano wa Iran na Uturuki na pili ni 'Kikao cha Viongozi wa Ubunifu wa Astana."

Balozi Farazvand amesema katika kipindi hiki nyeti na chenye kuainisha hatima ya eneo na dunia, mji mkuu wa Iran, Tehran utakuwa mwenyeji wa vikao hivyo viwili muhimu vya kimataifa ambavyo havijafanyika kwa muda mrefu.

Mkutano wa nchi zinazofanya juhudi za kurejesha amani huko Syria ambazo ni Iran, Russia na Uturuki tangu dunia ikumbwe na janga la corona hazijawahi kuitisha kikao cha ana kwa ana cha viongozi wa nchi hizo huku marais wa nchi tatu wakisisitiza juu ya udharura wa kukutana ana kwa ana kutokana na umuhimu wa kadhia zinazojadiliwa.