Amir-Abdollahian na Miqdad: Kuna ulazima wa kuheshimu mamlaka ya kujitawala Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i86100-amir_abdollahian_na_miqdad_kuna_ulazima_wa_kuheshimu_mamlaka_ya_kujitawala_syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Feisal Miqdad wameshiriki katika kikao cha pamoja na waandishi habari na kusisitiza kuhusu kulindwa mamlaka ya kujitawala Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 20, 2022 23:44 UTC
  • Amir-Abdollahian na Miqdad: Kuna ulazima wa kuheshimu mamlaka ya kujitawala Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Feisal Miqdad wameshiriki katika kikao cha pamoja na waandishi habari na kusisitiza kuhusu kulindwa mamlaka ya kujitawala Syria.

Miqdad aliwasili Jumatano mjini Tehran na baada ya kumalizika mazungumzo yake na Amir-Abdollahian walishiriki katika kikao cha pamoja na waandishi habari. Katika kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria kufanyika 'Kikao cha Astana' mjini Tehran Jumane ambacho kiliitishwa kujadili mchakato wa amani Syria na kilihudhuriwa na marais wa Iran, Russia na Uturuki na kusema: "Kikao hicho kilijaribu kuiondoa Syria katika hali ya kivita na kijeshi na kutatua masuala ya nchi hiyo kisiasa."

Aidha Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa, Iran inalitazama kwa umuhimu mkubwa suala la ulazima wa kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala Syria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha wasiwsi kuhusu uwezekano wa Uturuki kuingia kijeshi katika ardhi ya Syria na kuelezea matumaini yake kuwa, ushauri uliotolewa na nchi washiriki wa  'Kikao cha Astana' mjini Tehran utazingatiwa na wakuu wa Uturuki.

Mkutano na waandishi habari wa marais wa Russia, Iran na Uturuki baada ya kikao cha Astana cha mchakato wa amani wa Syria

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aidha amesisitiza kuwa,  wanajeshi vamizi wa Marekani wanapaswa kuondoka mara moja na bila masharti katika ardhi ya Syria.

Kwa upande wake Feisal Miqdad Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa jitihada zake hasa kuhusu taarifa ya mwisho ya 'Kikao cha Astana' ambayo imesisitiza kuhusu kulindwa mamlaka ya kujitawala Syria. Amesema  serikali ya Damascus inapinga hatua yoyote ya Uturuki kuingiza askari wake nchini Syria.

Kuhusu uwepo wa majeshi ya Marekani mashariki mwa Mto Furati, amesema Marekani haina haki ya kupora utajiri wa Syria.