Iran yasisitiza utatuzi wa kisiasa kwa mgogoro wa Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i86186-iran_yasisitiza_utatuzi_wa_kisiasa_kwa_mgogoro_wa_ukraine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo ya simu na mwenzake wa Hungary kuhusu uhusiano wa pande mbili na mgogoro wa Ukraine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 23, 2022 02:44 UTC
  • Iran yasisitiza utatuzi wa kisiasa kwa mgogoro wa Ukraine

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo ya simu na mwenzake wa Hungary kuhusu uhusiano wa pande mbili na mgogoro wa Ukraine.

Katika mazungzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amesisitiza kuhusu 'suluhisho la kisiasa' kwa mgogoro wa Ukraine na kusema Jamhuri ya Kiislamu inaendelea kushauriana na Russia na Ukraine ili kufikia lengo hilo. 

Aidha amesema Iran kimsingi inapinga vita na vikwazo na kuongeza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuhusu suluhisho la kisiasa la kutatua mgogoro wa Ukraine na kuhusiana na hilo inaendeleza jitihada na mashauriano baina ya Moscow na Kyiv ili kuimarisha na kuendeleza kasi ya suluhisho la kisiasa kwa mgogoro huo."

Hali kadhalika amesema Iran inasaidia kuhakikisha kuwa kuna usalama wa nishati na chakuka duniani kote baada ya vita vya Ukraine na kwamba tayari Tehran inafanya mazungumzo na Russia pamoja na Ukraine kuhusu suala hilo.

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo hayo, Amir-Abdollahian amesema Iran inataka kustawisha miradi yake ya nyuklia kwa malengo ya amani sambamba na kuondolewa vikwazo na kwa msingi huo inataka mapatano imara kwa upatanishi wa Umoja wa Ulaya.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Hungary Péter Szijjártó ameipongeza Iran kwa jitihada zake za kuleta uthabiti katika eneo na dunia nzima na kuongeza kuwa: "Tunataka amani Ukraine na eneo la Mashariki ya Kati na kuhusiana na hilo, tunaishukuru Iran kwa jitihada zake za kuleta uthabiti katika eneo na kuandaa Mkutano wa Astana mjini Tehran."

Aidha amesema, Hungary kama nchi jirani ya Ukraine inahisi hatari zinazotokana na kuendelea mgogoro katika nchi hiyo na imekumbwa na wimbi kubwa la wakimbizi na hivyo inataka vita vimalizike haraka iwezekanavyo.