Borrell: Shinikizo la vikwazo vya juu kabisa dhidi ya Iran limefeli
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amekiri kuwa sera ya shinikizo la kiwango cha juu zaidi dhidi ya Iran imefeli na kugonga mwamba.
Katika andiko lake lililochapishwa kwenye toleo la jana la gazeti la Financial Times, Borrell amesema kuhusu mazungumzo ya kuiondolea vikwazo Iran kwamba, utekelezaji kamili wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA uliathiriwa mno na hatua aliyochukua aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump ya kujitoa kwenye makubaliano hayo na kuanza kutekeleza sera ya upande mmoja ya "kampeni ya shinikizo la kiwango cha juu kabisa".
Katika sehemu nyingine ya andiko lake hilo, Mkuu wa Sera za Nje wa EU ameeleza kuwa shinikizo la kiwango cha juu kabisa limefeli. Huku akidai kwamba wanachama waliosalia kwenye JCPOA walifanya juhudi za kuyalinda na kuyadumisha makubaliano hayo, Borrell amesema wananchi wa Iran wamenyimwa manufaa kamili ambayo ilipasa wayapate kwa kuondolewa vikwazo.

Josep Borrell ameendelea kueleza kile alichodai kuwa ni jitihada alizofanya za kuongoza mazungumzo ya Vienna ya uondoaji vikwazo kwa kusema: "baada ya miezi 15 ya mazungumzo ya papo kwa papo na yenye nia ya kujenga ya mjini Vienna na mashauriano mengi niliyofanya na pande husika katika JCPOA pamoja na Marekani, nimefikia hitimisho kwamba anga ya ziada ya kufikia suluhu juu ya masuala muhimu imefikia tamati."
Aidha amedai kwamba: "nikiwa msahilishaji wa mazungumzo, kwa uoni wangu matini hii ndio makubaliano bora kabisa yanayoweza kufikiwa".
Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jambo linaloweza kutoa hakikisho la kufikiwa makubaliano thabiti na endelevu ni kuondolewa kiuhalisia vikwazo vyote na kuwepo dhamana ya Iran kupata manufaa na maslahi yake katika makubaliano hayo; na ndio maana Tehran imewasilisha mapendekezo na ubunifu unaotakikana kufanyiwa kazi ili uweze kufikiwa mwafaka katika mazungumzo.../