Iran: Tunafuatilia kwa karibu na kwa hisia kali matukio ya Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i86502-iran_tunafuatilia_kwa_karibu_na_kwa_hisia_kali_matukio_ya_iraq
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amegusia matukio ya nchini Iraq na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inafuatilia matukio hayo kwa kina, kwa karibu na kwa hisia kali; na inasisitiza kuwa, mazungumzo ndiyo njia pekee ya kuweza kutatua matatizo ya ndani ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 01, 2022 04:14 UTC
  • Iran: Tunafuatilia kwa karibu na kwa hisia kali matukio ya Iraq

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amegusia matukio ya nchini Iraq na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inafuatilia matukio hayo kwa kina, kwa karibu na kwa hisia kali; na inasisitiza kuwa, mazungumzo ndiyo njia pekee ya kuweza kutatua matatizo ya ndani ya nchi hiyo.

Nasser Kan'ani Chafi amesema hayo leo Jumatatu katika kikao chake cha kila wiki na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa, usalama wa Iraq ni usalama wa Iran na ni usalama wa eneo hili zima.

Ameongeza kuwa, mirengo, vyama, taasisi na makundi yote ya kisiasa yanaweza kutatua matatizo yao kwa kuheshimu katiba na kutumia njia za kisheria na si kwa kufanya fujo.

Amesema, njia ya utatuzi wa mgogoro wa Iraq ni kuchunga amani na kila upande kuuheshimu upande mwingine na pia kuundwa serikali ya wananchi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya kudumu ya nchi hiyo.

Maandamano nchini Iraq

 

Aidha amesema, Iran itaendelea daima kuheshimu chaguo la wananchi wa Iraq na kusisitiza kuwa, mazungumzo ndiyo njia bora kabisa ya kutatua matatizo ya nchi hiyo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amezungumzia pia mazungumzo ya Vienna ya mapatano ya nyukklia ya JCPOA na na kusema kuwa, Tehran muda wote imekuwa ikiheshimu mazungumzo nayo kwani shabaha yake hasa ni kuhakikkisha kunafikiwa makubaliano mapana, ya kudumu na yatakayodhamini manufaa ya taifa la Iran hasa ya kiuchumi.