Eslami: Viwanda na teknolojia ya ulinzi ya Iran iko mbele muda wote
Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran amesisitiza kuwa, viwanda vya silaha na sekta ya teknolojia ya ulinzi ya Iran daima iko mstari wa mbele.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Mohammad Eslami akisema hayo pambizoni mwa maonyesho ya Wizara ya Ulinzi yaliyohusiana na uzalishaji na uchumi unaotokana na mashirika yanayotegemea elimu kama msingi wake mkuu wa uzalishaji bidhaa na kusema kuwa, muda wote sekta ya ulinzi na kutumiwa teknolojia za kisasa katika sekta hiyo ni vipaumbele vikuu vya nchi zote ulimwengu na Iran pia ni hivyo hivyo.
Amesema, kwa taufiki ya Allah na kwa miongozo ya busara ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, sekta hiyo ya ulinzi iko mstari wa mbele pia katika taasisi na mashirika yanayotegemea elimu kama mtaji wake mkuu.
Mkuu huyo wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran vile vile amesema, licha ya kuweko vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa Tehran, lakini taifa hili la Kiislamu halijavunjika moyo kabisa, bali limejipinda kufanya utafiti wa kina wa sekta mbalimbali na limefanikiwa kuwa na uwezo imara na wa kujitegemea wa kuunganisha teknolojia na uzalishaji bidhaa.
Vile vile amesema, uwezo huo wa Iran ni mkubwa hivi sasa kiasi kwamba unaweza kujumuishwa kwenye sekta zote humu nchini.