Satalaiti ya Iran ya Khayyam yaendelea kutuma data
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i86878-satalaiti_ya_iran_ya_khayyam_yaendelea_kutuma_data
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia wa Iran Issa Zarepour ametangaza kuwa satalaiti ya Kiirani ya Khayyam ambayo Jumanne ilipaa kuelekea anga za mbali jana ilituma data mara nne kama ilivyotarajiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 10, 2022 22:54 UTC
  • Satalaiti ya Iran ya Khayyam yaendelea kutuma data

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia wa Iran Issa Zarepour ametangaza kuwa satalaiti ya Kiirani ya Khayyam ambayo Jumanne ilipaa kuelekea anga za mbali jana ilituma data mara nne kama ilivyotarajiwa.

Siku ya Jumanne, Satalaiti ya Iran ya Khayyam ilirushwa katika anga za mbali kwa kutumia roketi la Russia la Soyuz-2.1b na kuelekea umbali wa kilomita 500 kutoka ardhini. Hii  ni hatua mpya ya uhusiano wa kistratijia baina ya Tehran na Moscow katika masuala ya anga za mbali.

Satalaiti ya Khayyam imefikishwa katika anga za mbali kwa roketi hilo la Russia ambalo nalo limerushwa kutokea Kituo cha Baikonour Cosmordome nchini Kazakhstan ambacho kinasimamiwa na Russia.

Akizungumza Jumatano Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia wa Iran alisema: "Leo tumepokea taarifa kutoka satalaiti ya Khayyam mara nne katika Shirika la Anga za Mbali la Iran (ISA) kupitia kituo chake cha anga za mbali cha Mahdasht."

Aidha amesema Iran inaendelea kutengeneza satalaiti zingine kama hiyo ya Khayytam kwa ushirikiano na Russia. Amesema ni fahari kubwa kwa wataalamu wa Iran kufanya kazi pamoja na wataalamu wa Russia ambao wana uzoefu wa zaidi ya miongo sita katika uga wa anga za mbali.

Roketi la Soyuz likiwa linalekea anga za mbali likiwa limesheheni satalaiti ya Iran ya Khayyam

Hapo jana pia Rais wa Iran alisema kurushwa katika anga za mbali kwa mafanikio satalaiti ya Iran ya Khayyam ni chemichemi ya fahari na nguvu za Jamhuri ya Kiislamu.

Rais Ebrahim Raisi wa Iran alisema hayo katika kikao cha Baraza la Mawaziri na kuongeza kuwa, karibuni hivi taifa hili litashuhudia mafanikio makubwa katika anga za mbali.

Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa, kuanza kupokea data muhimu kutoka kwenye satalaiti hiyo iliyoundwa na wataalamu wa humu nchini ni fahari kubwa isiyo na kifani kwa taifa hili la Kiislamu.