Mamilioni ya watoto kupata chanjo ya Malaria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i87152-mamilioni_ya_watoto_kupata_chanjo_ya_malaria
Kampuni ya kutengenza dawa za binadamu ya GSK imepatiwa kandarasi ya kuzalisha chanjo ya kwanza ya Malaria duniani lengo likiwa ni kulinda mamilioni ya watoto dhidi ya ugonjwa huo unaopelekea mamilioni ya watoto kupoteza maisha, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 18, 2022 03:28 UTC
  • Mamilioni ya watoto kupata chanjo ya Malaria

Kampuni ya kutengenza dawa za binadamu ya GSK imepatiwa kandarasi ya kuzalisha chanjo ya kwanza ya Malaria duniani lengo likiwa ni kulinda mamilioni ya watoto dhidi ya ugonjwa huo unaopelekea mamilioni ya watoto kupoteza maisha, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Zoezi  hilo la kihistoria, litakalogharimu takriban dola milioni 170, litapelekea kupatikana kwa dozi milioni 18 za chanjo ya RTS,S katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, na uwezekano wa kuokoa maelfu ya maisha ya watoto kila mwaka.

Malaria inasalia kuwa moja ya ugonjwa mkubwa unaoua watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano. Mwaka 2020, takriban watoto nusu milioni wavulana kwa wasichana walikufa kutokana na ugonjwa huo barani Afrika pekee, idadi ambayo ni sawa na kifo kimoja kila dakika.

Etleva Kadilli, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ugavi cha UNICEF, amesema kandarasi hiyo inatuma ujumbe wa wazi kwa watengenezaji wa chanjo ya malaria kuendelea na kazi yao.

“Tunatumai huu ni mwanzo tu. Ubunifu unaoendelea unahitajika ili kutengeneza chanjo mpya na za kizazi kijacho ili kuongeza usambazaji unaopatikana, na kuwezesha soko bora la chanjo," amesema na kuongeza kuwa "Hii ni hatua kubwa imepigwa katika juhudi zetu za pamoja za kuokoa maisha ya watoto na kupunguza mzigo wa malaria kama sehemu ya mipango pana ya kuzuia na kudhibiti malaria."

Mbu anayeeneza Malaria

Malaria husababishwa na vimelea na huambukizwa kwa binadamu kupitia mbu jike aina ya Anopheles. Ingawa ugonjwa huo unaweza kuzuilika na kutibika, unaweza kusababisha kifo usipotibiwa.

Chanjo ya majaribio ilizinduliwa katika programu ya majaribio ya 2019, iliyoratibiwa na WHO, katika nchi tatu za Ghana, Kenya na Malawi  na hadi sasa imefikia zaidi ya watoto 800,000.

Mwezi Oktoba 2021, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa lilipendekeza matumizi yake makubwa katika nchi zenye maambukizi ya wastani hadi ya juu ya malaria.