Jeshi la Iran kufanya maneva ya kijeshi ya droni
(last modified Wed, 24 Aug 2022 04:18:57 GMT )
Aug 24, 2022 04:18 UTC
  • Jeshi la Iran kufanya maneva ya kijeshi ya droni

Jeshi la Iran leo Jumatano linatazamiwa kuzindua luteka ya kijeshi itakayohusisha ndege zisizo na rubani (droni).

Hayo yamesemwa na Admeri Habibollah Sayyari, Naibu Mratibu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye ameeleza kuwa, matawi yote manne ya jeshi la Iran yatashirikishwa kwenye mazoezi hayo ya kijeshi.

Admeri Sayyari amebainisha kuwa, maneva hayo yanaanza sambamba na kuanza Wiki ya Kitaifa ya Serikali hapa nchini, na yatafanyika katika pembe zote za Jamhuri ya Kiislamu.

Ofisa huyo mwandamizi wa jeshi la Iran ameongeza kuwa, droni 150 zilizozalishwa na wataalamu wa Iran wakishirikiana na mashirika ya wanataaluma ya hapa nchini zitarushwa na kufanyiwa majaribio katika luteka hiyo.

Droni za kijeshi za Iran

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa ni moja ya nchi chache duniani ambazo zinaendelea kupiga hatua mbele katika ubunifu, upanuzi na uundaji wa aina tofauti za ndege zisizo na rubani.

Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC alisema hivi karibuni kuwa: "huko nyuma, sisi hatukuwa na uwezo tulionao leo hii, na hivi sasa tunauza nje ya nchi makombora na ndege zisizo na rubani."