Iran: Nguvu zetu za kijeshi na kiulinzi si kitu cha kujadiliwa kabisa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i87770-iran_nguvu_zetu_za_kijeshi_na_kiulinzi_si_kitu_cha_kujadiliwa_kabisa
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Jeshi la Iran amesema kkuwa, nguvu za kiulinzi za Jamhuri ya Kiislamu si kitu cha kujadiliwa kabisa na kusisitiza kuwa, Iran itaendelea kuimarisha nguvu zake za kiulinzi kwa kiwango chochote inachokiona kinafaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 03, 2022 22:07 UTC
  • Iran: Nguvu zetu za kijeshi na kiulinzi si kitu cha kujadiliwa kabisa

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Jeshi la Iran amesema kkuwa, nguvu za kiulinzi za Jamhuri ya Kiislamu si kitu cha kujadiliwa kabisa na kusisitiza kuwa, Iran itaendelea kuimarisha nguvu zake za kiulinzi kwa kiwango chochote inachokiona kinafaa.

Brigedia Jenerali Amir Hatami amesema hayo na kuongeza kuwa, nguvu za taifa lolote lile zinategemea uwezo na uimara wake katika masuala ya kisiasa, kijeshi, kiuchumi na kijamii.

Amesema, majeshi ya Iran yanaelewa vyema uhalisia wa mambo ulivyo katika medani tofauti na kwamba vikosi hivyo vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu vinaendesha mikakati yake kwa kutegeea teknolojia za kisasa zilizopo na kufanya ubunifu na kutafuta teknolojia mpya kila siku kwa ajili ya kuimarisha mikakati yake hiyo. Lengo lake kuu ni kumarisha na kunyanyua juu nguvu za kitaifa za kijeshi na za kiulinzi za Iran.

Brigedia Jenerali Amir Hatami

 

Mshauri huyo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya jeshi la Iran pia amesema, vikwazo vya madola ya kiistikbari dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu vimetoa fursa ya kudhihiri na kutekelezwa kivitendo vipaji na ubunifu wa wataalamu wa ndani ya Iran ambao wamefanikiwa kuondoa matatizo na kulidhaminia taifa mahitaji yake ya kiufundi na kiulinzi. Sasa hivi wataalamu wa Iran wanajitengenezea wenyewe vipuri vinavyohitajiwa na jeshi la nchi kavu, mifumo ya makombora pamoja na ulinzi wa anga na wa baharini kwa gharama ndogo kabisa na kwa kutumia uwezo wa kielimu na bidii kazini.

Ikumbukwe kuwa, msingi mkuu wa siasa za kiulinzi za Iran ni kumzuia adui hata asifikirie kulishambulia taifa hili na siasa hizo zimekuwa zikifuatiliwa kwa njia mbalimbali humu nchini.