Iran: Tutaendelea na siasa za kustafidi na teknolojia mpya ikiwemo ya nyuklia
Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuimarishwa vinu vya atomiki na uzalishaji wa umeme wa nguvu za nyuklia ni katika malengo ya kutumia Iran haki yake ya kufaidika na tenkonolojia hiyo ya kisasa na lengo lake kwa sasa ni kuongeza matumizi ya umeme wa nyukia kwa asilimia 20.
Mohammad Eslami amesema hayo na kuongeza kuwa, hivi sasa kuna mashindano makubwa ya maendeleo ya teknolojia mpya kati ya madola makubwa duniani na katika siku zijazo dunia itashuhudia hali nzito ya ushindani huo.
Ameongeza kuwa, inasikitisha kuona kwamba, fikra iliyopo duniani hivi sasa kuhusu nishati ya nyuklia na vituo vyake ni ni fikra kwamba vituo hivyo ni vya kijeshi vyenye ulinzi mkali na masuala ni ya kijeshi wakati si hivyo. Adui naye anafanya njama za kila namna kukuza fikra hiyo na kutia hofu na kuvunjika moja watu kwa shabaha ya kuizuia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isiwe na ushawishi wala isiwe dola lenye nguvu duniani.
Eslami ameongeza kuwa, fikra hiyo ya kujaribu kuonesha kila kinachohusiana na nyuklia ni silaha, inaonekana pia katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Katika kipindi cha miaka yote hii, wakala huo umekuwa ukieneza hofu na kujaribu kuwapokonya watu moyo wao wa kujiamini kwa shabaha ya kudhoofisha mori wa wananchi wa Iran, ndio maana miongoni mwa ajenda kuu za Jamhuri ya Kiislamu ni kukabiliana na njama hizo na kuingiza matumaini na kujiamini kitaifa, katika nyoyo za wananchi wa Iran.
Amesisitiza kuwa, siasa za kufungua milango kwa ajili ya teknolojia mpya za kisasa ni miongoni mwa vipaumbele vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na itaendelea na siasa zake hizo kwa nguvu zote.