Ndege za Russia zinafanyiwa ukarabati nchini Iran
Ndege za abiria za Russia zinakarabatiwa nchini Iran huku uhusiano wa nchi hizi mbili jirani ukizidi kuimarika ili kukabiliana na vikwazo vya vya Marekani.
Waziri wa uchukuzi wa Iran Rostam Qassemi amesema Russia imeziagiza kampuni za usafiri wa anga za Iran kuzifanyia ukarabati ndege zake.
Qassemi amesema kwamba tayari ndege tisa za abiria za Russia ziko Iran kwa ajili ya kupata matengenezo huku akipigia debe teknolojia iliyopo katika sekta ya usafiri wa anga ya Iran ambayo imewezesha ukarabati na ukaguzi wa aina mbalimbali za ndege za abiria.
"Tumekuwa katika nafasi nzuri katika miezi ya hivi karibuni katika suala la ukarabati wa ndege," amesema waziri bila kufafanua aina za ndege za Russia zinazokarabatiwa nchini Iran.
Tangazo hilo linakuja huku kukiwa na ripoti za ushirikiano wa karibu kati ya Iran na Russia ili kupunguza athari za vikwazo vya madola ya Magharibi.
Mamlaka za Russia zimetangaza mara kadhaa kwamba Moscow imekuwa ikitumia uzoefu wa makampuni ya Iran na mashirika ya serikali katika kukabiliana na vikwazo vya madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani.
Iran na Russia zimetia saini mikataba mikubwa katika miezi ya hivi karibuni ili kuimarisha ushirikiano wao wa kiuchumi, kibiashara na nishati.
Marekani iliiwekea Iran vikwazo shadidi mnamo 2018 baada ya Washington kujiondoa kwa upande mmoja katika makubaliano ya kimataifa juu ya mpango wa nyuklia wa Iran.
Marekani na washirika wake waliiwekea Russia vikwazo vikali zaidi mwezi Februari baada ya Moscow kuanzisha operesheni ya kijeshi nchini Ukraine.

Wataalamu wanasema vikwazo vya Marekani vilishindwa kufikia lengo kuu la kuilazimisha Iran kulegeza misimamo yake imara katika masuala ya kisiasa na kijeshi. Wanasisitiza kuwa marufuku hiyo hata iliipa Iran fursa ya kubuni misingi ya uchumi wake mbali na mapato ya mafuta ghafi na kutegemea zaidi rasilimali zake za ndani.
Rais wa Russia Vladimir Putin alisema siku ya Jumatano wakati wa kongamano la kiuchumi huko Vladivostok kwamba nchi yake inapata faida kutokana na vikwazo vya Magharibi, akisema Moscow iliona fursa zaidi za kuingia katika masoko ya Mashariki ya Kati na Iran baada ya vikwazo hivyo.