Iran yaitaka Troika ya Ulaya kutofuata njia ya utawala haramu wa Israel
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taarifa iliyotolewa na Troika ya Ulaya inayojumuisha mataifa ya Uingereza, Ujerumani na Ufaransa kuhusiana na mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA na kutoa tuhuma dhidi ya Tehran haijengi na ni kinyume kabisa na nia njema.
Nasser Kanani Chafi amezinasihi nchi hizo tatu za Ulaya akiziambia kwamba, badala ya kuingia katika anga ya uharibifu wa kidiplomasia zije na njia ya utatuzi ya kuhitimisha hitilafu za kimtazamo zilizobakia kuhusiana na mazungumzo ya nyuklia.
Kanani amesema hayo katika radiamali yake kwa taarifa ya madola hayo kuhusiana na mazungumzo ya kuondolewa vikwazo Iran na kueleza kwamba, inasikitisha kuona kuwa taarifa hiyo inatolewa katika mazingira ambayo kumekuwa na ushirikiano wa kidiplomasia na pande husika zimekuwa zikibadilishana na jumbe na taarifa mbalimbali kwa ajili ya kufikia natija ya mazungumzo ya Vienna.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kusema kuwa, inasikitisha mno kuona kwamba, Troika ya Ulaya inatoa taarifa isiyo na kipimo na hivyo kufuata njia ya utawala haramu wa Israel ya kusambaratisha mazungumzo na hapana shaka kuwa, endapo mwenendo huu utaendelea, basi madola hayo yanapaswa kubeba dhima na masuuliya ya natija ya hili.
Nasser Kanani Chafi amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ingali ina nia, irada na utayari kamili kwa ajili ya kufikiwa natija ya mwisho katika mazungumzo hayo na inaamini kwamba, endapo kutakuweko na azma na irada ya kweli na ya lazima na wakati huo huo pande husika kutoathiriwa na mashinikizo kutoka nje, basi kuna uwezekano wa kufikiwa makubaliano kwa haraka mno.