Iran: Tuko tayari kuendelea kushirikiana ipasavyo na IAEA
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ujerumani na Ufaransa zinapaswa kurekebisha misimamo yao, zifuate njia sahihi ya mazungumzo hayo na ziangalie mambo katika uhalisia wake.
Nasser Kan'ani amesema hayo leo Jumatatu katika mazungumzo yake ya kila wiki na waandishi wa habari ambapo huwa anatumia fursa hiyo kutangaza na kutoa ufafanuzi kuhusu siasa za mambo ya nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesema, Iran kimaumbile ni nchi muhimu sana katika soko kubwa la nishati duniani na uwezo wake huo unalifanya taifa hilo kupigiwa mahesabu muhimu na madola ya dunia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amesema, hatua ya nchi tatu za Ulaya ya kutoangalia mambo katika uhalisia wake ni kwa madhara ya nchi hizo.
Ameongeza kuwa, Iran inafanya juhudi zake zote kuyafanya mazungumzo yanayoendelea huko Vienna yafikie makubaliano ya mwisho. Lakini mapatano ni kitu cha pande mbili na kinachotarajiwa ni kuona pande nyingine za mazungumzo nazo zinaonesha nia ya kweli ya kufanikisha makubaliano ya mwisho.
Amma kuhusu maadhimisho ya Arubaini ya Imam Husain AS huko Karbala Iraq, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, licha ya kujitokeza baadhi ya matatizo kama vile joto kali mno lakini wapenzi wa Imam Husain na Ahlul Bait wa Mtume Muhammad SAW wanaendelea kushiriki kwa mamilioni katika ziara ya Arubaini huku wengine wakijitolea kila kitu chao kuwahudumia wafanya ziara hao huko Iraq.