Rais Raisi: Haiwezekani kufikia makubaliano bila faili la Iran katika IAEA kufungwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i88394-rais_raisi_haiwezekani_kufikia_makubaliano_bila_faili_la_iran_katika_iaea_kufungwa
Rais Ebrahim Raisi amesema, haiwezekani kufikia makubaliano ya nyukllia bila faili la Iran katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kufungwa; na akaongeza kwamba, Ulaya inapaswa ionyeshe kivitendo kuwa sera zake hazina mfungamano na Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 20, 2022 22:39 UTC
  • Rais Raisi: Haiwezekani kufikia makubaliano bila faili la Iran katika IAEA kufungwa

Rais Ebrahim Raisi amesema, haiwezekani kufikia makubaliano ya nyukllia bila faili la Iran katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA kufungwa; na akaongeza kwamba, Ulaya inapaswa ionyeshe kivitendo kuwa sera zake hazina mfungamano na Marekani.

Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Jumatatu aliondoka Tehran kuelekea New York kwa ajili ya kushiriki katika kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Ayatullah Sayyid Ebrahim Raisi amesema katika mazungumzo na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kuwa, Iran iko tayari kufikia makubaliano ya kiuadilifu, thabiti na endelevu, na akabainisha kuwa sharti la kufikiwa makubaliano hayo ni Tehran kupatiwa dhamana za uhakika na kufungwa mafaili yanayohusiana na shughuli zake za nyuklia.
Rais wa Iran amesema: kiwango cha ushirikiano na uhusiano kati ya Iran na Ufaransa kinaweza kustawishwa, na kwamba Ulaya inatakiwa ionyeshe kivitendo kwamba ina sera huru na wala haifuati matakwa na sera za Marekani.
Katika mazungumzo hayo Ayatullah Raisi ameashiria kujitoa Marekani katika mapatano ya JCPOA na pia kutotekeleza nchi za Ulaya ahadi zao za kuhakikisha Iran inanufaika kutokana na mapatano hayo na akaongezea kwa kusema: kutokana na hatua ya upande mmoja ya Marekani ya kujiondoa katika makubaliano na hasara zilizosababishwa na hatua hiyo, takwa la Jamhuri ya Kiislamu la kupatiwa dhamana zenye uhakika linakubalika kikamilifu kiakili na kimantiki.

Rais wa Iran ameendelea kueleza kwamba kubakishwa wazi mafaili ya Iran katika wakala wa IAEA ni kizuizi kikubwa cha kufikiwa makubaliano na akasema: “mtazamo wa IAEA juu ya masuala inapasa uwe wa kiufundi bila kuathiriwa na mashinikizo na ushawishi wa watu wengine. Amesisitiza kwa kusema: "tunaamini kuwa haiwezekani kufikia makubaliano bila mafaili ya Iran kufungwa."

Katika mazungumzo hayo, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, alitoa mapendekezo kadhaa kwa ajili ya mazungumzo yanayoendelea hivi sasa na akakiri kwa kusema: ni ukweli kwamba wakati IAEA ilitangaza kuwa Iran ilitekeleza majukumu yake kikamilifu, mwaka 2018 Marekani ilijitoa katika JCPOA na pande za Ulaya nazo pia hazikuweza kutimiza ahadi zao kuhusu kufaidika Iran na manufaa ya kiuchumi ya makubaliano ya JCPOA.
Aidha Macron alimwalika rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutembelea Ufaransa na akasema: tunaweza kuongeza ushirikiano wetu kwa kupanua uhusiano wa pande mbili na wa masuala ya kiuchumi na kikanda.../