"Maadui wanataka kukwamisha ustawi wa Iran katika uga wa sayansi"
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89516-maadui_wanataka_kukwamisha_ustawi_wa_iran_katika_uga_wa_sayansi
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema ghasia zilizoshuhudiwa hapa nchini zilipangwa na kuchochewa na maadui, kwa shabaha ya kukwamisha ustawi wa Jamhuri ya Kiislamu katika uga wa sayansi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 21, 2022 00:43 UTC

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema ghasia zilizoshuhudiwa hapa nchini zilipangwa na kuchochewa na maadui, kwa shabaha ya kukwamisha ustawi wa Jamhuri ya Kiislamu katika uga wa sayansi.

Brigedia Jenerali Hossein Salami alisema hayo jana Alkhamisi akihutubia mkusanyiko wa wanafunzi na wanazuoni wa Chuo cha Kidini Cha Qum, kusini mwa Tehran na kuongeza kuwa, "Adui anataka kulemaza ustawi wa Iran, na ndio maana wamejaribu kuvuruga shughuli katika Vyuo Vikuu, hii inaonesha wanataka kukwamisha ustawi wa Iran katika uga wa sayansi."

Kamanda Salami ameeleza kuwa, "Mpango wa Marekani ni kufunga Vyuo Vikuu na shule zetu, kwa kuwa inafahamu vyema kuwa sayansi na maarifa zinapatikana katika taasisi hizo za elimu."

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu anasisitiza kuwa, Wamarekani wamejaribu kuwarubuni vijana wa Kiirani na kuwashawishi waupinge Mfumo unaotawala hapa nchini, lakini hatimaye wamegundua kuwa vijana hao hawawezi kufanywa wapumbavu na Marekani.

Maajenti kadhaa wa Wamagharibi wamekamatwa hapa nchini kwa kuchochea ghasia

Jenerali Salami ameashiria mafanikio ya kiraia na kijeshi ya Iran katika kuzalisha ndege zisizo na rubani (droni) na kutuma satalaiti katika anga za mbali na kubainisha kuwa, Uistikbari wa Dunia unatumia vita laini na vya kisaikolijia ili kuuangusha Mfumo wa Kiislamu na kulipigisha magoti taifa la Iran kupitia mashinikizo, lakini ndoto yao hiyo kamwe haitatimia.  

Wamagharibi wanaunga mkono na kuchochea ghasia ambazo zimekuwa zikishuhudiwa hapa Iran kwa kisingizo cha kuaga dunia Mahsa Amini, mwanamke Muirani aliyezirai katika kituo cha polisi na kisha kupoteza maisha wakati akiwa anapata matibabu hospitalini mwezi uliopita.