Watu 10 watiwa nguvuni nchini Iran kwa tuhuma za kushirikiana na MOSSAD
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i89660-watu_10_watiwa_nguvuni_nchini_iran_kwa_tuhuma_za_kushirikiana_na_mossad
Kitengo cha Habari cha Idara ya Mahakama ya Iran kimetangaza kutiwa nguvuni watu 10 kwa tuhuma za kushirikiana na shirika la ujasusi la Israel (MOSSAD).
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Oct 24, 2022 22:55 UTC
  • Watu 10 watiwa nguvuni nchini Iran kwa tuhuma za kushirikiana na MOSSAD

Kitengo cha Habari cha Idara ya Mahakama ya Iran kimetangaza kutiwa nguvuni watu 10 kwa tuhuma za kushirikiana na shirika la ujasusi la Israel (MOSSAD).

Watu hao 10 wametajwa kuwa maajenti wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao kazi yao kuu ilikuwa kubaini maafisa wa intelijinsia wanaofanya kazi katika mkoa wa Azarbaijan Magharibi. 

Kitengo cha Habari cha Idara ya Mahakama ya Iran kimeripoti kuwa, wanachama wa kundi hilo huku wakiongozwa moja kwa moja na maafisa wa kijasusi wa shirika la Mossad, walikuwa wakifanya kazi ya kuwatambua maafisa wa intelijinsia ambao walikuwa wakifanya kazi katika Idara ya Usalama wa Taifa; na lengo lao lilikuwa ni kuchota  taarifa kutoka kwa wafanyakazi hao wa intelijinsia kwa kuwateka nyara, kuwatishia na kuwapiga. Maajenti hao wa kundi hilo aidha walikuwa wakiwasiliana moja kwa moja na maafisa wa shirika la Mossad. 

Watu hao waliotiwa mbaroni kwa tuhuma za kushirikiana na Mossad walikuwa wamepokea pesa mara kadhaa kutoka kwa maajenti ya utawala wa Kizayuni na maafisa wa Mossad kutokana na kazi waliyokuwa wamezifanya hadi sasa.  

Majasusi hao walikuwa wakiwasiliana moja kwa moja kwa njia ya video na maafisa wa Mossad huku wakifanya kazi waliyotumwa katika mikoa ya Azerbaijan Magharibi, Tehran na Hormozgan.

Majasusi hao wa Mossad pia katika baadhi ya matukio, walijaribu hata kuwaua maafisa usalama na upelelezi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, njama ambayo halikufanikiwa.