Kukiri Grossi kuhusu kutokuwepo mpango wa kijeshi wa nyuklia nchini Iran
Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA akijibu swali kuhusu uwezekano wa Iran kupata bomu la nyuklia amesema: "Katika kiwango cha sasa cha uzalishaji urani iliyorutubishwa, Iran imeweza kuzalisha kiwango cha kutosha cha kuiwezesha kutengeneza zaidi ya kifaa kimoja (cha mlipuko) iwapo itataka kufanya hivyo."
Rafael Grossi bila kupoteza muda ameongeza: "Pamoja na hayo lakini hatuna habari yoyote inayoonyesha kwamba Iran hivi sasa ina mpango wa kijeshi wa nyuklia. "Mkurugenzi Mkuu wa IAEA amekiri kwamba hakuna mpango wowote wa kijeshi wa nyuklia unaotekelezwa nchini Iran katika hali ambayo Wamagharibi wamekuwa wakitekeleza siasa za kuishinikiza Iran kupitia wakala huo wa nyuklia, na hatua za Grossi pia zimeongeza uchochezi wao katika uwanja huu.
Miongoni mwa hatua hizo ni kupitishwa tarehe 17 Novemba azimio lililopendekezwa na Marekani na Troika ya Ulaya katika Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ikiwa ni katika kuendeleza siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu na kuelekezwa tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Waandaaji wa azimio hilo ambalo lilipingwa na China na Russia walitoa tuhuma bandia na siziso na msingi kuhusu kugunduliwa mada za nyuklia katika maeneo matatu ambayo hayakutangazwa awali nchini Iran na kuitaka serikali ya Tehran ishirikiane zaidi na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia katika uwanja huo. Ni miaka mingi sasa ambapo Wamagharibi wamekuwa wakiituhumu Iran, bila kutoa ushahidi wala uthibitisho wowote wa kuaminika, kuwa ina silaha za nyuklia, na kwa msingi huo kuchukua hatua za kisiasa na kutekeleza vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran.

Msemaji wa Ikulu ya White House Karin Jean-Pierre alidai mnamo Agosti 2022 kwamba: "Rais Biden amethibitisha kuwa anataka kuizuia Iran kumiliki silaha za nyuklia".
Kwa hakika, kinyume na tuhuma hizo zisizo na msingi za Wamagharibi kuhusiana na juhudi za Tehran za kutengeneza silaha za nyuklia, Iran imeweza kutumia teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani katika nyanja mbalimbali zikiwemo za uzalishaji umeme, dawa, matibabu na kilimo.
Pejman Shirmardi, Naibu Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran anasema: Iran imefanikiwa kujitosheleza katika uzalishaji wa zana za teknolojia ya nyuklia. Mafanikio ya Shirika la Nishati ya Atomiki ni kadi ya ushindi kwa timu ya mazungumzo. Hofu kubwa ya upande wa mazungumzo wa Magharibi ni elimu na maarifa (teknolojia) asilia yanayopatikana nchini.
Suala ambalo Marekani na waitifaki wake wa Ulaya pamoja na utawala wa Kizayuni daima wamekuwa wakihofia ni kuzidi kuimarika uwezo wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani. Malengo hayo ya mpango wa nyuklia wa Iran yamethibitishwa mara nyingi katika ripoti zinazotolewa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki. Ni wazi kuwa jambo linalozidisha wasiwasi unaodaiwa na Marekani na washirika wake ni hatua za Iran baada ya Marekani kujitoa katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia mashuhuri kwa jina la JCPOA.
Hata kama Iran kwa miaka kadhaa ilijitolea kutekeleza kikamilifu ahadi zake za nyuklia na kupunguza shughuli zake katika uwanja huo, katika fremu ya makubaliano hayo, lakini katika kipindi cha urais wa Donald Trump mnamo Mei 2018, Merikani iliamua kujiondoa kwa upande mmoja katika makubaliano hayo na kuanza kutekeleza vikwazo vikali zaidi dhidi ya Iran katika kile kilichotajwa kuwa mashinikizo ya juu zaidi na ya kulemaza dhidi ya mfumo wa Kiislamu.
Kwa upande mwingine, kutokana na uvunjwaji wa mara kwa mara wa ahadi za wanachama wa Umoja wa Ulaya wa kundi la 4+1 katika kutekeleza ahadi zao, Tehran kwanza ilianza kupunguza ahadi zake za nyuklia katika hatua 5 na kisha, sambamba na kutekeleza sheria iliyopitishwa na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) ya Iran katika uwanja huo, ikaamua kuchukua hatua mpya katika kustawisha mradi wake wa nyuklia kwa malengo ya kiraia.

Miongoni mwa mambo yanayoweza kuashiriwa katika muktadha huu ni kurutubishwa urani kwa kiwango cha asilimia 20 na kisha asilimia 60, maandalizi ya urani chuma na kuongezwa taasisi na suhula za nyuklia, jambo ambalo limeitia wasiwasi mkubwa Washington na washirika wake wa kieneo hususan utawala wa Kizayuni. Kupungwa kiwango cha ushirikiano na wakala wa IAEA kwa kusimamishwa utekelezaji wa protokali ziada pia kumeongezwa katika utekelezaji wa sheria iliyopitishwa na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na katika kukabiliana na hatua ya nchi za Ulaya ya kutotekeleza ahadi zao kwa Iran.
Bila shaka, Iran imetangaza mara kadhaa wakati wa kufanyika mazungumzo ya kuiondolea vikwazo huko Vienna Austria kwamba iko tayari kutekeleza kikamilifu majukumu yake ya JCPOA iwapo masharti iliyotoa, ikiwa ni pamoja na kuondolewa vikwazo na kurejea Marekani katika mapatano ya JCPOA, yatatekelezwa kikamilifu.