Kan'ani: Palestina itabakia milele; kuangamia ni katika dhati na utambulisho wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i92298-kan'ani_palestina_itabakia_milele_kuangamia_ni_katika_dhati_na_utambulisho_wa_israel
Msemaji wa Wizara vya Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa radiamali kwa madai yasiyo ya msingi ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel na kueleza kuwa, hatua hiyo inafuatilia kujijengea utambulisho wake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 30, 2022 09:03 UTC
  • Kan'ani: Palestina itabakia milele; kuangamia ni katika dhati na utambulisho wa Israel

Msemaji wa Wizara vya Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa radiamali kwa madai yasiyo ya msingi ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel na kueleza kuwa, hatua hiyo inafuatilia kujijengea utambulisho wake.

Nasser Kan'ani Chafi amebainisha kuwa, Palestina haiwezi kuangamia bali, suala la kuangamia na kusambaratika lipo katika dhati na utambulisho wa utawala ghasibu wa Israel.

Akijibu madai ya Netanyahu, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter: Kwa zaidi ya miaka 70 sasa Israel imekuwa ikihaha ili ijinasue kutoka katika kinamasi cha mgogoro wa utambulisho wake ambao umeambatana na mauaji ya umati, uporaji mali, kuwalazimisha Wapalestina kuwa wakimbizi na makumi ya hatua nyingine za ukiukaji wa haki za binadamu ambazo ni tafsiri ya sera na hatua ghalati za Uingereza, Marekani na baadhi ya madola ya Ulaya yanayounga mkono uwepo huu usio halali wa utawala bandia wa Israel.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa kibaguzi wa Israel alitangaza Alkhamisi ya jana kwamba, moja ya majukumu makuu ya serikali yake eti ni kuizuia Iran isiiangamize Israel na kudai kwamba, serikali hiyo itafanya jitihada za kuizuia Tehran isifanikiwe kufikia uundaji wa silaha za nyuklia.

Baraza la mawaziri la Netanyahu jana Alkhamisi lilipata kura ya kuwa na imani nalo katika Bunge la Israel (Knesset). Huko nyuma Netanyahu amewahi kuhudumu katika nafasi ya Waziri Mkuu wa Israel kwa miaka 15, lakini hili linachukuliwa kuwa baraza lake la mawaziri lenye misimamo mikali zaidi katika historia yote ya utawala wa Kizayuni.