Makundi mawili ya kigaidi yatokomezwa kaskazini magharibi mwa Iran
Vikosi vya nchi kavu vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) la Sepah vimeyasambaratisha na kuyatokomeza makundi mawili ya kigaidi huko kaskazini magharibi mwa nchi karibu na mpaka wa Iraq na kuwaangamiza magaidi kadhaa.
Kamanda wa vikosi vya nchi kavu vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour amesema kupitia taarifa kwamba makundi hayo mawili ya kigaidi yalijaribu kujipenyeza na kuingia nchini kupitia eneo la mpakani la Oshnavieh kwa lengo la kufanya hujuma na mashambulio ya kigaidi.
Jenerali Pakpour amesema, mapigano kati ya askari wa Sepah na magaidi hao yaliendelea kwa saa kadhaa ambapo magaidi 12 waliangamizwa na askari watatu wa jeshi hilo waliuawa shahidi katika mapambano hayo.
Ameongeza kuwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu linaendelea na operesheni ya kuyatokomeza mabaki ya magaidi hao katika eneo hilo.
Katika operesheni hiyo, jeshi la Sepah limenasa pia silaha kadhaa, zana na nyaraka za magaidi hao.
Brigedia Jenerali Mohammad Pakpour hakubainisha utambulisho wa magaidi hao lakini kwa kawaida uvamizi na mashambulio ya aina hiyo katika eneo la kaskazini magharibi mwa Iran huwa yanafanywa na kundi la PJAK ambalo ni tawi la kundi la PKK linaloendesha harakati zake ndani ya ardhi ya Uturuki na Iraq.
Mashambulio ya kigaidi ni nadra kutokea nchini Iran, lakini makundi ya kigaidi yenye mfungamano na al-Qaeda huwa baadhi ya wakati yanafanya mashambulio ya kuvizia na kukimbia.../