Faini ya dola bilioni 18 inaisubiri Pakistan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i94766-faini_ya_dola_bilioni_18_inaisubiri_pakistan
Onyo lililotolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba kama serikali ya Pakistan haitochukua msimamo ulio wazi kuhusu mkataba wa kununua gesi kutoka Iran, basi kuna hatari Islamabad ikalazimika kulipa faini ya dola bilioni 18. Inaonekana wazi kuwa, viongozi wa Pakistan wamelichukulia kwa uzito onyo hilo.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Mar 05, 2023 22:58 UTC
  • Faini ya dola bilioni 18 inaisubiri Pakistan

Onyo lililotolewa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba kama serikali ya Pakistan haitochukua msimamo ulio wazi kuhusu mkataba wa kununua gesi kutoka Iran, basi kuna hatari Islamabad ikalazimika kulipa faini ya dola bilioni 18. Inaonekana wazi kuwa, viongozi wa Pakistan wamelichukulia kwa uzito onyo hilo.

Karibu miaka 10 imepita tangu mradi wa kujenga bomba la gesi baina ya Iran na Pakistan ulipoanza kutekelezwa kivitendo kufuatia makubaliano ya pande mbili. Pakistan inahitajia mno gesi ya Iran kwa ajili ya matumizi yake ya nishati, hivyo pande mbili zilikubaliana kujenga bomba la gesi ambalo litarahisishia Islamabad kununua gesi ya Iran. Kwa upande wake, Iran imetekeleza ahadi zake na kutokana na kuchunga kwake ujirani mwema, hadi hivi sasa imesita kuishitaki Pakistan kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake kwa mujibu wa mkataba huo. Lakini inaonekana kuwa, muda mrefu umepita na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiwezi tena kuvumilia.

Hivi sasa suala hilo limefika mpaka kwenye vyombo vya habari vya Pakistan ambavyo vimetangaza kuwa, inavyoonekana serikali ya Pakistan hususan Idara ya Mahesabu imeogopeshwa na onyo hilo la Iran na imezihimiza mamlaka husika za Pakistan kulitatua suala hilo.

Ujenzi wa bomba la gesi baina ya Iran na Pakistan

 

Suroush Amiri, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitoa pendekezo la kujengwa bomba la gesi la amani kwa ajili ya kusaidia utulivu na usalama katika eneo zima la Asia Magharibi. Hivi sasa na baada ya kutiliana saini mkataba na Pakistan kuhusu suala hilo, Tehran imetekeleza jukumu lake la kulifikisha bomba hilo la gesi kwenye mipaka ya Pakistan, lililobakia ni viongozi wa Islamabad kutekeleza ahadi zao kwa mujibu wa mkataba huo.

Inavyoonekana ni kuwa, Tehran kamwe haikufikiria kwamba Islamabad ingekwenda kinyume na mkataba ilioutia saini kwa hima na hamu kubwa. Hasa kwa kutilia maana kuwa Pakistan inahitajia mno nishati na kimsingi gesi ya Iran ni ya bei nafuu mno kwake kuliko gesi ya nchi yoyote ile. Lakini moja ya sababu kuu zilizowafanya viongozi wa Pakistan wakwame katika mpango wao wa kununua gesi kutoka Iran, ni mashinikizo ya Marekani na kukubali kwake kuburuzwa na dola hilo  la kibeberu la Magharibi.

Serikali ya Pakistan inaifuata Marekani katika siasa zake dhidi ya Iran kiasi kwamba hivi sasa kuna taarifa kuwa Islamabad imekusudia kuwasilisha kwa ubalozi wa Marekani onyo hilo la Iran la kuishitaki Islamabad na uwezekano wa Pakistan kupigwa faini ya dola bilioni 18 kwa kwenda kinyume na mkataba wake. Lakini Pakistan ni nchi huru, hivyo si laiki kwake hata kidogo kujadiliana na dola jingine kuhusu mustakbali wa wananchi wake.

Bendera za Iran na Pakistan

 

Kimsingi ni Pakistan ndiyo inayohitajia nishati, lakini Marekani inaikwamisha nchi hiyo kama sehemu ya kufanikisha siasa zake za kibeberu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Wataalamu wa uchumi na siasa wa Pakistan wanasema kuwa, kuendelea kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani si kwa manufaa ya Islamabad. Bali itibari ya serikali ya nchi hiyo inazidi kupotea mbele ya wananchi na wanaiona Pakistan imegeuzwa kuwa nchi tiifu kwa Marekani na haishughulishwi haiguswi na matatizo makubwa ya nishati ya wananchi wake.

Bahram Zahedi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Viongozi wa serikai ya Pakistan wametangaza mara chungu nzima kwamba, wanataka kuwa na ushirikiano wa karibu na wa pande zote kati yao na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hasa katika masuala ya nishati, lakini hawachukua hatua yoyote ya kivitendo ya kufanikisha jambo hilo.

Kiujumla ni kwamba, ni haki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kushindwa kuvumilia kutokana na kurefuka mno ufanikishaji wa ahadi za Pakistan katika mkataba wa bomba la gesi. Iran imewekeza fedha nyingi katika mradi huo na hadi hivi sasa imeonesha nia nzuri ya ujirani mwema kwa kutoishitaki serikali ya Islamabad, lakini sasa subira yake imeisha hasa kutokana na viongozi wa Pakistan kuonesha wanakubali kuchezewa na Marekani.

Hii ni katika hali ambayo, mikataba yote ya kimataifa inakuwa na sheria zake maalumu zinazotambuliwa kimataifa. Serikali ya Pakistan haiwezi kukwepa majukumu yake muda wote kuhusu mkataba huo. Hivi karibuni Tehran imeitaka Islamabad ichukue msimamo wa wazi kuhusu suala hilo ili Iran iweze kujua nini cha kufanya. Iran nayo ina hamu ya kuona mkataba huo unatekelezwa na haipendi hata kidogo kuona jirani yake anapigwa faini ya mabililoni ya dola.