Amir Abdollahian: Mlango wa mazungumzo ya nyuklia hautabakia wazi milele
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i95602-amir_abdollahian_mlango_wa_mazungumzo_ya_nyuklia_hautabakia_wazi_milele
Hossein Amir Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema rasimu ya mpango wa kuainisha kiwango cha mazungumzo ya nyuklia inajadiliwa katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) na kusisitiza kwamba mlango wa mazungumzo hayo hautabakia wazi milele.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 28, 2023 03:43 UTC
  • Amir Abdollahian: Mlango wa mazungumzo ya nyuklia hautabakia wazi milele

Hossein Amir Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema rasimu ya mpango wa kuainisha kiwango cha mazungumzo ya nyuklia inajadiliwa katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) na kusisitiza kwamba mlango wa mazungumzo hayo hautabakia wazi milele.

Mazungumzo magumu ambayo yamekuwa yakiendelea kwa miezi kadhaa huko Vienna, Austria kwa lengo la kuindolea Iran vikwazo vya kidhalimu ilivyowekewa na nchi za Magharibi, yamefikia hatua ambayo iwapo Marekani ikiwa nchi iliyokiuka mapatano ya nyuklia mashuhuri kama JCPOA, itakubali matakwa halali na yenye mantiki ya Iran katika uwanja huo, basi makubaliano ya mwisho yanaweza kufikiwa haraka.

Uzoefu wa mazungumzo ya miezi kadhaa huko Vienna umethibitisha kwamba Ikulu ya Marekani haina uwezo wa kuamua kurejea kwenye makubaliano hayo ya nyuklia kutokana na matatizo ya ndani na mashinikizo ya utawala wa Kizayuni, na kwa mtazamo huo imekuwa ikitumia mbinu za kuilamu Iran bila sababu zozote za msingi  na kuiwekea makataa bandia.

Mazungumzo ya JCPOA mjini Vienna

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa masharti ya kuhakikishiwa kivitendo kuwa vikwazo vitaondolewa, kupata dhamana kuhusu uthabiti wa mapatano ya JCPOA na kuondolewa madai yasiyo na msingi ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki  IAEA, kama matakwa yake makuu katika mazungumzo hayo.

Akizungumza hivi karibuni na televisheni ya al-Jazeera ya nchini Qataer, Hossein Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, amesema Iran itaendelea kuheshimu mashirikiano yake na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema, Qatar daima imekuwa na mwelekeo sahihi na kwamba imekuwa na nafasi muhimu chanya katika kufanikisha mazungumzo ya kubadilishana wafungwa kati ya Iran na Marekani na vilevile mazungumzo ya nyuklia kwa ujumla wake.