Jun 20, 2016 07:04 UTC
  • Iran yatibua shambulizi la kigaidi dhidi ya Tehran

Vyombo vya usalama nchini Iran vimetibua njama ya kutekelezwa shambulizi la kigaidi hapa mjini Tehran na kuwatia mbaroni watuhumiwa kadhaa wa njama hizo za kigaidi.

Hayo yamebainishwa na Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye ameongeza kuwa, magaidi hao wamekamatwa na vyombo vya usalama hapa nchini katika kipindi cha siku chache zilizopita. Amesema kuwa magaidi hao walikuwa wanapania kufanya hujuma za kigaidi katika maeneo tofauti ya mji mkuu Tehran, wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Jumatatu iliyopita, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran IRGC lilitekeleza operesheni maalumu na kuangamiza timu ya magaidi watano wa kundi la kigaidi la PJAK kaskazini magharibi mwa nchi. Taarifa ya IRGC ilisema magaidi hao waliuawa kufuatia operesheni maalumu ya kikosi cha nchi kavu cha jeshi hilo karibu na mji wa Sardasht, ambapo wanajeshi wa Iran walifanikiwa kunasa silaha kadhaa na nyaraka za siri.

Mwezi uliopita wa Mei, Mahmoud Alavi, Waziri wa Usalama wa Iran alisema vikosi vya usalama nchini vinafuatilia kikamilifu nyendo za maadui wanaopanga kufanya hujuma za kigaidi katika ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu na kwamba maafisa usalama nchini hadi sasa wamefanikiwa kusambaratisha makundi 20 ya kigaidi.

Tags